CCM yatumia kete tatu kupata ushindi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka mkakati wa kutumia maeneo matatu ya kuwaomba kura wagombea wa chama hicho katika ngazi zote ili kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Dk Bashiru Ali amesema maeneo hayo yatawezesha mgombea wa urais wa Tanzania, urais Zanzibar, ubunge, uwakilishi na udiwani kupata ushindi.

“Tutapita kila mahali, nyumba kwa nyumba, shina kwa shina, tawi kwa tawi, kata kwa kata, tarafa kwa tarafa, wilaya kwa wilaya, kitanda kwa kitanda tukifafanua ubora na uwezo wa wagombea wetu katika ngazi zote za urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, urais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wabunge na madiwani,” amesema Dk Bashiru wakati wa mkutano wa kampeni za Samia mjini Dodoma.

Ameongeza: “Nikuhakikishie mheshimiwa mgombea wetu na Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) kwamba mwaka huu ushindi utakuwa mkubwa kuliko wakati wowote wa uchaguzi katika mfumo wa vyama vingi na sababu si nyingine ni kwamba tumesimamisha wagombea bora.”

SOMA: CCM imepata nyota watatu kuangaza uchaguzi 2025

Dk Bashiru ametaja eneo la pili ni kutetea rekodi ya utendaji wa CCM kwa miaka mitano iliyopita hasa kwa kutilia mkazo kazi zilizofanywa na ahadi walizoziahidi mwaka 2020.

Kiongozi huyo ambaye ni sehemu ya waratibu wa kampeni za mwaka huu amesema eneo la tatu ni kutangaza kwa ufasaha yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030 katika ngazi ya taifa, mikoa na wilaya.

Dk Bashiru amesema tofauti na kampeni za mwaka 2020, mwaka huu Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imetengeneza kanda 11 za kampeni za chama hicho.

“Mwaka 2020 tulikuwa na utaratibu na wewe (Rais Samia) ulifanya kazi hiyo ukiongozwa na Dk John Magufuli na Mheshimiwa Kassim Majaliwa, mwaka huu Halmashauri Kuu ya CCM imeboresha imetengeneza kanda 11 nchi nzima,” amesema.

Dk Bashiru amesema yeye na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wanaongoza kampeni katika kanda ya kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora na akasema kanda hiyo itahakikisha inaongoza kwa kuwapa kura nyingi wagombea wa chama hicho.

Aidha, mgombea urais kupitia CCM, anatarajiwa kufanya mikutano mikubwa ya kampeni katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.

Kwa upande wa Mkoa wa Songwe, Shamrashamra za kishindo cha mapokezi ya mgombea wa CCM zimetikisa kwa zaidi ya wananchi 20,000 wameshiriki matembezi na mbio fupi kumuunga mkono kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoufungua Mkoa wa Songwe.

Matembezi na mbio hizo vilifanyika katika miji ya Tunduma na Vwawa jana, zikihusisha makundi ya vijana, akinamama na wazee.

Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Songwe, Yusuph Rajabu alisema wananchi wanachama na wakereketwa wa CCM katika miji hiyo wamepanga kuvunja rekodi ya kuhudhuria kwa wingi kumsikiliza mgombea urais wa CCM.

“Songwe ndilo lango kuu la biashara katika ukanda wa SADC, hatuna jambo dogo, leo (jana) tumefanya mbio fupi katika mji wa Tunduma ikiwa ni maandalizi ya kumpokea kiongozi wetu ambapo zaidi ya watu 10,000 wameshiriki,” amesema Rajabu.

Ameongeza: “Pia mchana tumeshiriki matembezi maalumu katika mji wa Vwawa ambako watu zaidi ya watu 12,000 wameshiriki. Tumejipanga kuweka rekodi ya kipekee katika mikutano yote ambayo mgombea wetu, Rais Samia atafanya kampeni zake”.

Rajabu amesema wananchi wa Songwe wako tayari kumpokea mgombea huyo kwa kishindo kwa sababu ameleta neema ya maendeleo na kuufungua mkoa huo.

Amesema katika miaka minne ya Rais Samia madarakani Songwe imepiga hatua za maendeleo katika sekta za afya kwa kujengwa hospitali ya rufaa ya mkoa.

“Kabla ya kujengwa hospitali, wanaSongwe walilazimika kwenda Mbeya kupata huduma za rufaa, lakini sasa huduma zote tunazipata hapa,” amesema Rajabu.

Ameongeza: “Mwaka 2020 tulikuwa na hospitali mbili za wilaya lakini sasa zipo tano, majengo matatu ya huduma za dharura katika hospitali ya rufaa yameanza kutoa huduma na zahanati zimeongezeka kutoka 155 mwaka 2020 hadi kufikia 214 zilizopo sasa sawa na ongezeko la zahanati 55”.

Rajabu amesema Rais Samia ameongeza watumishi wa afya kutoka 570 hadi 1,350 likiwa ni ongezeko la  watumishi 780 na nyumba za watumishi zimeongezeka kutoka 322 hadi 922.

“Mimi ni mwalimu kitaaluma, katika sekta ya elimu, Rais Samia ameweka rekodi ya kipekee kwani idadi ya shule za msingi zimefikia 532 kutoka 455, shule za sekondari zimefikia 155 kutoka shule 120 na hata madarasa yalikuwa 3,600 lakini sasa yamefikia 4,272,” amesema.

Akizungumzia ahadi 13 ambazo Rais Samia aliahidi kuzitekeleza ndani ya siku 100 akichaguliwa, Rajabu amesema suala la ajira 500 kwa sekta ya afya na 7,000 kwa walimu wa hisabati na sayansi zitaongeza wigo wa ajira kwa vijana na kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika masomo hayo.

Amesema ahadi ya kutoa mtaji wa Sh bilioni 200 kwa wafanyabiashara wadogo, imewagusa wajasiriamali wa mkoa huo kwani wanaamini watakwenda kuongeza wigo wa mitaji yao kibiashara.

Rajabu alisema suala la wahitimu wa mafunzo stadi kupata maeneo ya kuendeleza ujuzi wao, itawasaidia vijana kuendeleza ujuzi wao na kujiajiri kupitia taaluma walizozipata.

“Mama hana deni bali sisi anatudai, maandalizi yamefanyika, wananchi wana matumaini makubwa hivyo tutampigia kura za heshima. Mkoa wa Songwe katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwaka jana, tulishika nafasi ya nne kitaifa. Sasa kwa jambo hili la mama tunakwenda kushika nafasi ya kwanza kwa wingi wa kura za Rais,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button