CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinastahili kuitwa ‘Kiona Mbali’ maana kimeona mbali kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 20, 2025 na kupata ‘nyota tatu.’
Mwishoni mwa wiki CCM kilikuwa katika Mkutano Mkuu Maalumu ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wa ngazi mbalimbali katika chama.
Kimsingi, CCM imefanya mambo makubwa matatu ambayo ni kuona mbali ndio maana ninasema, CCM inafaa kuitwa ‘Kiona Mbali.’
Katika kujiandaa vyema na kuingia sawia katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wakati ukifika, kupitia Mkutano Mkuu wa Januari 18 na 19, mwaka huu CCM kimekumbuka ukweli kuwa, ng’ombe hanenepi siku ya mnada.
Mambo hayo matatu ni kwanza, kimeziba pengo la nafasi ya uongozi lililokuwa wazi baada ya kujiuzuru Makamu Mwenyekiti wa CCM Kitaifa (Tanzania Bara), Abdularhman Kinana Julai, 2024.
SOMA: Kishindo Mkutano Mkuu CCM leo
Chama Cha Mapinduzi ‘kimemvalisha viatu’ vya Kinana kada mkongwe wa siasa, Stephen Wazira. Sasa, CCM kinaongozwa na Rais Samia (Mwenyekiti wa Kitaifa), Makamu Mwenyekiti Zanzibar ni Dk Hussein Mwinyi (Rais wa
Zanzibar), Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara (Stephen Wasira) na Katibu Mkuu, Dk Emmanuel Nchimbi.
Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara ni John Mongella na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar ni Dk Mohamed Said Dimwa. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa ni Amos Makalla.

Jambo la pili ambalo pia ni miongoni mwa mambo ninayoita nyota, ni kupokea taarifa za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (ZSM) kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.
Ripoti hizo kama zilivyowasilishwa na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa SMZ, Hemed Suleiman Abdulla zinaonesha kama si ‘kulamba dume’, basi chama tawala (CCM) ‘kimelamba turufu’ katika utekelezaji huo.
Kimsingi, mafanikio makubwa yanaonekana katika maendeleo ya kiuchumi; miradi ya maendeleo, maendeleo ya uwekezaji na upatikanaji wa ajira ama za moja kwa moja, au zisizo za moja kwa moja sambamba na maendeleo makubwa ya huduma za kijamii.
Hongera CCM maana ‘mnatoka katika vita ya 2020 mkiwa mmeshikilia kitu mkononi’ (utekelezaki wa ilani) na mtaingia katika ‘vita’ Oktoba 2025, mkiwa na ‘silaha za kisiasa mkononi’ na si maneno matupu ambayo hata kwenye kanga yapo.
Nyota ya tatu kati ya nyota zilizong’aa katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliofanyika hivi karibuni Dodoma,
ni kutokana na ‘nyota tatu’ nyingine zitakazowakilisha CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Mwaka 2025 kwa nafasi za kitaifa.

Kimsingi, CCM imeweka historia kwa kuwachagua wagombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu mapema na si bure, Kiona Mbali kimeona mbali.
CCM kimemteua Rais Samia (mwenyekiti) kuwa mgombea wa urais katika uchaguzi huo ujao na kumteua Dk Emmanuel Nchimbi (Katibu Mkuu) kuwa mgombea mwenza ambaye chama kitakaposhinda, basi ndiye atakayekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa sasa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni Dk Philip Mpango ambaye ameomba na kukubaliwa kuwa, kipindi hiki cha uongozi kikiisha, apumzike. Wakati hao wakiwa ‘nyota mbili’ za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, chama hicho kimemteua Dk Hussein Mwinyi (Makamu Mwenyekiti- Zanzibar) kuwa Mgombea Urais wa Zanzibar.
Kwa kufanya hivyo, tayari CCM imejitwalia nyota tatu zitakazoiangazia katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa ngazi ya kitaifa.
Faida nyingi kuliko hasara
Wadau mbalimbali wanaitaja hatua ya CCM kuweka wazi ‘Taa za Uchaguzi Mkuu’ kwa mitazamo tofauti huku baadhi wakisema si sahihi sana kwa kuwa hali hiyo inawaweka katika hatari mbalimbali zikiwamo za kiusalama na kisiasa kwani inaweka muda mrefu wa mtu kuingizwa katika ‘majaribu’ ya kusalitiwa, kuhujumiwa au yeye mwenye kusaliti au kuhujumu chama.
Wadau wengi wa siasa wanaunga mkono hatua hiyo inayotajwa kuwa ni kujiamini kisiasa kwa kuwa walioteuliwa wote ni wasafi ‘wasio na doa’ la kisiasa wala kimaadili na uzalendo wao kwa taifa, hautiliwi shaka.
Miongoni mwa sababu za kuunga mkono hatua hiyo ni kwamba, inaondoa tishio la kuwapo makundi ndani ya chama ambayo kila kundi linacheza bahati nasibu kuona ‘mtu wake anapitshwa.’
Kwa hatua hiyo, CCM imewafunga mdomo ‘wenye mdomo mrefu unaotoa udenda wanaposikia suala la madaraka.’
CCM sasa inabaki na kazi ya kuandaa au kukamilisha Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2025-2030 wanachama wakiwa na ‘sauti, jicho na ulimi’ mmoja.
Kimsingi wakati wanachama wa vyama vingine ‘wakiruka na kukanyagana’ kuteua wagombea huku kila mmoja akisikia harufu ya uchaguzi, chama tawala kitakuwa kinaendelea na jitihada za kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani maana ndicho chama tawala kilichoshika hatamu.
Kwamba, kitakuwa kinajitahidi kuhamasisha wanachama na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na ama kujiandikisha au kurekebisha taarifa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura shughuli ambayo inaendeleda hadi sasa chini ya Tume Huru ta Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Kadhalika wakati huo chama kitakuwa kinaendelea kuhamasisha wananchi kuhudhuria mikutano ya kampeni na kujitokjeza kupiga kura siku inapowadia.
Ndio maana kwa kuteua mapema wagombea wake, Chama Cha Mapinduzi kimejinyooshea mapito na kujiweka katika hali nzuri zaidi kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 kikiwa na bendera inayopepea kutangaza haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa na maendeleo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda ananukuliwa na HabariLEO akisema kutangaza wagombea mapema kunaepusha propaganda za watu watakaojaribu kumchafua mgombea kwa kuwa kunatoa muda wa kutosha kufafanua hoja zinazoibuka dhidi yake na kuhusu masuala mbalimbali.
Kwamba kwa kujulikana mapema, jamii hupata muda wa kutosha kumtathmini mgombea na kutoa fursa mapema
kufanyia kazi hoja zinazotolewa kuliko zinaposemwa kipindi hicho hicho cha uchaguzi.
Kimsingi, CCM wana mambo mengi yanayostahili kuigwa na vyama vingine haswa mtindo na mfumo wao wa kuachiana madaraka unaoonesha kuwa hakuna anayepaswa kung’ang’ania madaraka mithili ya kupe au ruba na
hakuna mwenyekiti wala mgombea wa kudumu katika chama.
Kimsingi baadhi ya vyama vya siasa huchelewa kubainisha wagombea kwani vingine huwa vinasubiri ‘kuokota masalia ya wanasiasa’ wanaoachwa na vyama vyao na kwa kuwa wana uchu wa madaraka, huamua kwenda kwingine ambako watakabidhiwa bendera kuzipeperusha.
Kimsingi, CCM kimepata nyota tatu zitakazopaswa kuendelea kuangaza mwanga wa amani na nuru ya upendo na matumaini zaidi. Ndio maana katika salamu zake za pongezi kwa wateule hao wa CCM, Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile anasema: “…TEF tunawapongeza viongozi hawa walioteuliwa na kuchaguliwa kwa nyadhifa hizi.”
Balile kwa niaba ya TEF anaongeza: “Matumaini yetu kama Jukwaa ni kuwa viongozi hawa wataendeleza jukumu la
kulitumikia taifa la Tanzania na kuwakomboa wananchi kutoka katika lindi la umaskini na kuwaletea maendeleo ya kweli.”
Anaongeza: “… Hongereni sana mlioteuliwa kwa nyadhifa hizo, tunatumaini Watanzania wakiwachagua katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu, mtaendeleza misingi imara ya nchi hii ya amani, upendo, utulivu, mshikamano na Muungano wa Tanzania.”
Kiu kubwa ya Watanzania baada ya uchaguzi Mkuu wa 2025 ni kuwa na viongozi wapenda watu, waadilifu, wapenda
maendeleo, wanaothamani maridhiano na uhimilivu pamoja na kutoa haki kwa usawa, amani, umoja na mshikanao wa kitaifa.