Nishati, JICA wajadili utekelezaji miradi

DODOMA: KATIBU  Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amekutana na wataalam kutoka Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kujadili hali ya utekelezaji wa miradi ya nishati inayofadhiliwa na shirika hilo.

Kikao hicho kimefanyika Septemba 8, 2025 katika ofisi za Wizara ya Nishati Mtumba jijini Dodoma.

Pande hizo mbili zilijadiliana kuhusu kuwajengea uwezo wataalamu wa Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika masuala ya kusanifu mitandao ya usambazaji wa gesi asilia.

Miradi iliyojadiliwa kwa kina katika kikao hicho ni wa kusafirisha umeme kutoka Tanzania hadi Uganda (UTIP) na mradi wa umeme Dodoma Ring Circuit unaolenga kuzidi kuimarisha hali ya upatikanaji umeme Dodoma.

Katika kikao hicho, Mramba ameisisitiza JICA kuhusu suala la utekelezaji mradi wa mfano wa usambazaji gesi asilia katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ambao utakuwa kielelezo cha manufaa ya gesi asilia iliyogunduliwa hapa nchini ambayo itasaidia pia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Vilevile, Mramba ameishukuru JICA kwa kufadhili miradi ya nishati ambayo imekuwa chachu ya maendeleo nchini hususan katika Jiji la Dodoma ambalo linaendelea kukua kwa kasi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button