Askari Magereza mbaroni akituhumiwa kuua mpenzi
ASKARI wa Jeshi la Magereza (31) jina limehifadhiwa anatuhumiwa kumuua mpenzi wake ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi, Bitie Chacha (25).
Mwalimu huyo mkazi wa Bugweto A, Kata ya Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga ameuawa kwa kuchomwa na chupa sehemu mbalimbali za mwili wake.
SOMA: Wahalifu 76 wakamatwa Shinyanga
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema Bitie aliuawa juzi saa moja usiku kwa kuchomwa kwa chupa mapajani, shingoni na kichwani.
Magomi alisema polisi huyo tayari wamemkamata mtuhumiwa huyo kwa mahojiano zaidi.
Alisema Bitie alikuwa akiishi na ofisa magereza huyo wakiwa ni wapenzi lakini walihitilafiana ndipo mtuhumiwa akamshambulia mwalimu huyo kwa kumchoma kwa vipande vya chupa shingoni, kichwani na mapajani.
“Tunahamasisha jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani vipo vyombo vya dola vimewekwa kutatua changamoto kwa maelewano,” alisema Magomi.
Alisema Jeshi la Polisi limekuwa likitoa elimu kwenye jamii kuhusu malezi kwenye familia ili kadiri miaka inavyokwenda kisiwepo kizazi kinachofanya vitendo vya kikatili.
Mmoja wa rafiki wa Bitie (jina limehifadhiwa) alidai ugomvi wa wapenzi hao ulianzia baa kwa kutuhumiana baada ya askari huyo kuchukua simu ya mkononi na kusoma ujumbe mfupi.
Baadhi ya majirani wa wapenzi hao, Sophia Tulipu na Saudia Gabriel walidai mwalimu huyo alikuwa akiishi na mtuhumiwa na mara kwa mara walikuwa wakigombana.



