RC Iringa aonya vyanzo vya maji visichezewe

IRINGA: Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameutaja mkoa wake “moyo wa Bonde la Rufiji” na kuhimiza ulinzi mkali wa zaidi ya vyanzo 440 vya maji vinavyolihudumia bonde hilo.
Ameonya kuwa uvamizi na matumizi yasiyo sahihi ya ardhi vinatishia uhai wa rasilimali hiyo muhimu kwa Taifa.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Kumi ya Maji Bonde la Rufiji, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa bodi hiyo mjini Iringa, RC James alisema Serikali itaendelea kuongeza nguvu katika kutunza vyanzo vya maji, ambapo tayari 74 vimewekwa kwenye mpango mahsusi wa uhifadhi.

Akifafanua zaidi, RC James alisema mabadiliko ya tabianchi, kilimo na ufugaji holela karibu na vyanzo vya maji ni kati ya changamoto zinazosababisha uchafuzi na upungufu wa maji katika maeneo mengi.
“Tunapaswa kuwa waangalifu sana. Kilimo na ufugaji usio rasmi karibu na vyanzo vya maji lazima ukomeshwe kwani madhara yake ni makubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho,” alisema RC James.

Alisema jamii inapaswa kuendelea kuelimishwa juu ya uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya maji ili kulinda vyanzo hivyo.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, David Mkyara, alisema Bonde la Rufiji linapita katika mikoa 11 nchini, lakini Iringa ndiyo pekee linalopitiwa kwa asilimia 100, jambo linaloufanya mkoa huo kuwa kitovu cha uhai wa mfumo wa maji katika bonde hilo.

“Tunahitaji jitihada za pamoja kuhakikisha rasilimali za maji zinalindwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,” alisema Mkyara.
Akaongeza kuwa usimamizi madhubuti wa vyanzo vya maji vya Iringa unachangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa Mto Rufiji na upatikanaji wa maji kwa mabwawa na maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.

Akiwasilisha taarifa ya utendaji wa bodi iliyomaliza muda wake, Mwenyekiti wa zamani, Naomi Lupimo, alisema katika kipindi cha uongozi wao wamefanikiwa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji na uhifadhi wa maji kwa kuhakikisha bwawa la Mto Nyerere linafikia ujazo unaotakiwa katika misimu ya mvua, tofauti na miaka ya nyuma ambapo mzunguko wa kujaza ulikuwa wa miaka mitatu.
Lupimo alitaja pia uwekezaji katika miundombinu, ikiwemo magari sita, pikipiki 16, baiskeli 16, mitambo mikubwa miwili, pamoja na kuimarishwa kwa ofisi za bodi katika mikoa mbalimbali, hatua iliyosaidia kuongeza ufanisi wa kazi.
Mjumbe wa bodi hiyo, Lucy Tewele, alisema uongozi mpya utaweka mkazo kwenye utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya maji, uhifadhi wa mazingira na umuhimu wa jamii kushiriki katika mipango ya ulinzi wa vyanzo vya maji.
Hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo inaashiria mwanzo mpya katika kulinda rasilimali za maji ndani ya Bonde la Rufiji, ambalo linachukua eneo la kilomita za mraba 183,791 — sawa na asilimia 20 ya eneo lote la Tanzania Bara.
Mto Rufiji, ambao ni mto mrefu zaidi nchini, hutiririsha maji kwenda Bahari ya Hindi na ni uti wa mgongo kwa uzalishaji wa umeme, kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya nyumbani.
Bonde hilo linahusisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Dodoma, Singida, Tabora, Morogoro, Ruvuma, Njombe, Lindi, Dar es Salaam na Pwani, huku Iringa ikibeba uzito zaidi kutokana na kuwa kitovu cha vyanzo vikuu vya maji kuelekea Rufiji.
Kwa hatua hii mpya, uongozi wa mkoa na bodi ya maji wanaamini kuwa mustakabali wa usalama wa maji nchini utazidi kuimarika endapo elimu, usimamizi na nidhamu ya matumizi ya maji vitapewa kipaumbele.



