Polisi waonya viongozi makundi ya WhatsApp

GEITA; JESHI la Polisi mkoani Geita limewataka viongozi wa makundi sogozi mtandaoni (WhatsApp) kuchukua hatua madhubuti kudhibiti usambazaji wa taarifa za uchochezi na uvunjifu wa amani.

Pia limewataka viongozi na watumiaji wote wa mitandao ya kijamii kutumia nafasi yao kudhibiti mitandao ya kijamii isiwe majukwa ya ukatili wa kijinsia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo ametoa maagizo hayo alipoungana na Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Geita kutoa msaada katika Kituo cha Afya Nyankumbu mjini Geita.

Kamanda Jongo amesema katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili jeshi la polisi linaendelea kuchukua hatua stahiki kukomesha vitendo vya ukatili kwa makundi yote wanawake na wanaume.

Amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni : “Ungana, Kutokomeza Unyanyasaji wa Kidijitali Dhidi ya Wanawake na Wasichana Wote” inapaswa kufanyiwa kazi na kila mtu ili iweze kuzaa matunda.

Amesema jeshi la polisi linaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya ufuatiliaji mtandaoni kuwakamata na kuwachukulia hatua wanaovunja sheria mtandaoni.

“Mpaka sasa kuna watuhumiwa watatu wa makosa ya kimtandao ambao tumewapeleka mahakamani, wapo ambao majalada yapo kwa mwanasheria kwa sababu ni makundi tofauti,” amesema Jongo.

 

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Geita, Grace Kaijage amesema ndani ya mwaka mmoja matukio ya ukatili mkoani Geita yamepungua kwa takribani asilimia 17.

“Mwaka jana (2024) makosa yaliyoripotiwa mkoa mzima yalikuwa 241 na kwa mwaka huu (2025) makosa yaliyoripotiwa yalikuwa 198, ambapo kuna upungufu wa zaidi ya makosa 43,” amesema

Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita, Lucy Beda amesema serikali imejizatiti kulinda usalama na kudhibiti ukatili wa kijinsia wa makundi yote bila kujali jinsia yake ili kutokomeza tatizo.

Awali Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyankumbu, James Joseph amekiri kupokea msaada wa mashuka na vifaa vya usafi vilivyotolewa na Mtandao wa Polisi Wanawake mkoa wa Geita ikiwa ni sehemu ya siku 16 za kupinga ukatili.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button