Aagiza ushirikiano watendaji taasisi zote zinazogusa afya

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Innocent Bashungwa ametaka kuimarishwa kwa mawasiliano na uhusiano baina ya watendaji wa serikali hasa waganga wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa wilaya na taasisi za kidini zinazotoa huduma za afya katika maeneo mbalimbali kwa wananchi.
Waziri Bashungwa alitoa kauli hiyo jijini hapa Jumatatu, baada ya Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristo nchini (TCMA), Dk Paul Kisanga kueleza katika risala kwamba kuna baadhi ya halmashauri zimekuwa zikishindwa kuhuisha mikataba ya vituo vya afya vya kanisa, hata pale ambapo bado kituo cha serikali hakijafikia kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa.
“Sitaki kusikia kuna mawasiliano na mahusiano hafifu kati ya waganga wakuu wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri na taasisi za dini ambazo zinatoa huduma za afya kwa wananchi,” alisema.
Akifungua mkutano huo wa 85 wa TCMA, alisema suala la uhusiano kati ya serikali na taasisi za dini ambazo zinatoa huduma za afya kwa wananchi ni muhimu.
Hivyo alimwagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe kuhakikisha ushirikiano baina ya pande mbili hizo unadumishwa.
“Sasa ni mkurugenzi gani wa halmashauri gani na DMO gani atakayepuuzia hili, kwa kweli atakuwa haitaki kazi hiyo. Haraka tuanzie hapo lakini sasa tuipe timu mapitio hayo ya mikataba waipitishe ili tukubaliane jinsi ya kulitekeleza,” alisema.
Serikali imekuwa ikifanya juhudi katika kuboresha sekta ya afya kwa kushirikiana na taasisi za dini ambapo katika kipindi cha mwaka 2021-2022 imetumia zaidi ya Sh bilioni 383 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati 564, vituo vya afya 304 na hospitali za wilaya 68.
“Sasa tukichukua takwimu hizi na kwenye upande wa taasisi za dini, rais wenu ametaja takwimu na mikataba ambayo tunajadili na kuhuisha itaenda kuboresha vituo vya tiba,” alisema.
Pia alisema Sh bilioni 103.09 zimetumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye zahanati vituo vya afya na hospitali za wilaya.
Alisema mwaka huu wa fedha serikali imetenga Sh bilioni 69.9 kwa ajili ya kuendelea kununua vifaa tiba.
“Jitihada kubwa zimekuwa zikifanyika katika kujenga miundombinu lakini bado tuna pengo ambalo tunaendelea kulijaza.
“Nitumie nafasi hii kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan hivi tunavyozungumza tumeshafanya na kukamilisha mikataba. Tupo katika hatua za manunuzi ya kununua vifaa tiba ikiwemo magari vyenye thamani ya Sh bilioni 149.5,” alisema.
Awali, Rais wa Chama cha Madaktari wa Hospitali za Mashirika ya Dini (TCMA), Dk Paul Kisanga alisema lengo la mkutano huo ni kujadili jinsi ya kuboresha huduma za afya na kukuza ushirikiano kati ya madaktari na watoa huduma pamoja na kubadilishana mawazo kutafuta njia za kutatua matatizo ya utoaji wa huduma.
“Kila mwaka inachaguliwa mada maalumu inayolengwa kwenye shabaha na mwaka huu tumelenga kwenye maboresho ya hospitali za kanisa katika utoaji wa huduma za afya na upatikanaji wa rasilimali fedha endelevu,” alisema.
Dk Kisanga alisema hospitali nyingi za makanisa zipo katika maeneo ya vijijini ambako ndiko walipo wananchi wengi na watu wenye uwezo mdogo wa kumudu hali ya maisha.