Abiria JNIA kunufaika huduma mpya za ukarimu

ONGEZEKO la idadi ya abiria wanaotumia viwanja vya ndege nchini limeendelea kuongeza umuhimu wa kuboresha huduma na mazingira ya kuwahudumia wasafiri, hususan katika viwanja vikuu vinavyounganisha Tanzania na mataifa mengine.
Kwa mujibu wa ripoti ya Tanzania in Figures 2025 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kwa kutumia takwimu za Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), idadi ya abiria wa ndani na kimataifa waliotumia viwanja vya ndege nchini iliongezeka kutoka milioni 7.38 mwaka 2024 hadi takribani milioni 8.11 mwaka 2025.
Katika idadi hiyo, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, ulihudumia takribani abiria milioni 2.92 mwaka 2025.
Ukuaji huo unaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha miundombinu na huduma za viwanja vya ndege ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya usafiri wa anga, utalii na shughuli za biashara.
Katika hatua hiyo, kampuni ya kimataifa ya Plaza Premium Group (PPG) imefungua eneo la mapumziko kwa wasafiri katika Terminal 3 ya JNIA, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kutoa huduma hiyo nchini Tanzania.
Eneo hilo lililopo karibu na Lango la 6 katika sehemu ya safari za kimataifa lina ukubwa wa mita za mraba 336 na uwezo wa kuhudumia watu 86 kwa wakati mmoja.
Huduma zinazopatikana ni pamoja na sehemu za kupumzika, kuoga, chakula na vinywaji, maeneo ya kufanyia kazi, intaneti, sehemu za kuchaji vifaa vya kielektroniki pamoja na vyumba vya ibada.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Makamu wa Rais wa Biashara wa Plaza Premium Group, Kanda ya Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika (EMEA), Anis Jmour, alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo nchini ni sehemu ya upanuzi wa shughuli za kampuni hiyo katika soko la Afrika Mashariki.
Alisema Tanzania ni soko lenye umuhimu katika kuunganisha safari za kikazi na mapumziko, hivyo kampuni inalenga kutoa huduma zinazozingatia mahitaji ya wasafiri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa JNIA, Bertha Bankwa, alisema kuongezeka kwa uwekezaji na huduma mpya katika viwanja vya ndege kunaonesha ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga nchini.
Alisisitiza kuwa kadiri idadi ya abiria inavyoongezeka, ni muhimu kuendelea kuboresha huduma ili kuhakikisha wasafiri wanapata mazingira yanayokidhi mahitaji yao wanapotumia viwanja vya ndege.
Ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga una umuhimu pia kwa uchumi wa taifa kutokana na mchango wake katika kurahisisha shughuli za biashara, kuvutia uwekezaji na kukuza utalii.
Tanzania inaendelea kupokea wageni wanaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro na Zanzibar, huku JNIA ikiwa miongoni mwa milango mikuu ya kuingia na kutoka nchini.
Plaza Premium Group ina uzoefu wa takribani miaka 30 katika sekta ya huduma za ukarimu viwanja vya ndege. Kampuni hiyo ilianzisha dhana ya lounge huru za viwanja vya ndege mwaka 1998 na kwa sasa inafanya shughuli zake katika viwanja vya ndege zaidi ya 600 katika nchi zaidi ya 150.
Katika huduma zake nchini Tanzania, kampuni hiyo imesema itazingatia pia utamaduni wa eneo husika kupitia mkakati wake wa Proudly Local, unaojumuisha vyakula na vitafunwa vya Kitanzania pamoja na bidhaa zinazopatikana nchini.



