Abuni mashine kuchakata mafuta ya parachichi

MASHINE rahisi isiyotumia umeme imebuniwa kwa lengo la kuchakata mafuta ya parachichi.

Mbunifu na Mtafiti kutoka Shirika la Utafiti na Maendeleo  ya Viwanda Tanzania (Tirdo), Paul Kipati amesema hayo alipozungumza na HabariLEO kuhusu kuongezea thamani zao la parachichi.

Amesema baada ya kugundua maparachichi mengi yanaharibika kwa kukosa soko, waliamua kubuni teknolojia hiyo itakayokuwa mkombozi kwa wakulima.

Advertisement

“Ikitokea soko ni zuri wakulima watauza parachichi, ikitokea soko sio zuri watatengeneza mafuta ambayo ni malighafi kwa bidhaa za urembo na usafi, malighafi kwa ajili ya mafuta ya kupikia na matumizi mengine mbalimbali.

“Kwa mfano mafuta ya parachichi unaweza kutumia kwa kutengenezea losheni, kupaka kwa ajii ya afya ya mwili, shampoo za kuoshea nywele, sabuni za kuogea hata kutumia kwa ajili ya kupikia zikitengenezwa katika hali ya usafi na ubora,” amesema.

Amesema mafuta hayo ya parachichi kitaalam yana vitamin A kwa wingi na vitamin E ambayo ni chakula cha ngozi pamoja na nywele.

“Kwa hiyo watengenezaji wengi wa vipodozi aina mbalimbali wanatumia mafuta haya kutengeneza  vipodozi vyao,” amesema.

Amesema hata baada ya kuchakata hilo parachichi, mbegu inayobakia ambayo hutupwa kama takataka na yenyewe ni bidhaa.

“Inatengeneza vinywaji mbalimbali,  mfano chai ukichanganya ile mbegu ya parachichi inakuwa ni chai bora inayotoa lehamu kwenye mwili, kusafisha tumbo na vitamin mbalimbali,” amesema.

4 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *