ACT-Wazalendo wataka marufuku nishati ya mafuta migodini

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeishauri serikali ibuni miradi mbadala ya nishati rafiki wa mazingira na itumike katika migodi yote ya uchimbaji madini ambayo bado haijaunganishwa na umeme wa gridi na ipige marufuku migodi kuendesha shughuli zake kwa kutumia nishati ya mafuta.

Ushauri huo umetolewa jana na chama hicho kupitia kwa Waziri Kivuli wa Madini wa chama hicho, Edgar Mkosamali katika taarifa yao ya ufuatiliaji wa vikao vya bunge vinavyoendelea mjini Dodoma.

Mkosamali alisema Aprili 27, mwaka huu, Waziri wa Madini, Doto Biteko aliwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

Advertisement

Katika mpango huo, pamoja na juhudi mbalimbali zilizofanywa kuinua sekta ya madini na pato lake kwa taifa, alisema bado kwenye suala la mazingira kuna changamoto za uharibifu na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike.

Alisema, Biteko katika kuwasilisha mpango wa makadirio ya mapato na matumizi, aliwasilisha baadhi ya tafiti za mazingira zilizofanywa zinazoonesha shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini huchangia kwa asilimia nne hadi saba katika uharibifu wa mazingira nchini.

Aidha, Mkosamali alisema utafiti wa ACT-Wazalendo walioufanya katika migodi mitano ya wachimbaji wadogo mkoani Mwanza na Geita, wamegundua kuna uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na ukataji miti kwa ajili ya nishati na magogo ya miti yanayosimikwa ili kusapoti njia za uchimbaji chini ya ardhi.

“Tofauti na migodi mikubwa inayotumia zege, wachimbaji wadogo hutumia maelfu ya magogo ya miti kwa ajili hiyo. Ukifika katika migodi ya wachimbaji wadogo utadhani umefika katika kiwanda cha kuchakata magogo,” alisema Mkosamali.

Katika hilo, alishauri Wizara ya Madini ishirikiane na wizara inayohusika na masuala ya mazingira, nishati, maji, ujenzi na afya katika kusimamia changamoto za miundombinu kwenye maeneo ya machimbo hasa ya wachimbaji wadogo na kuja na njia ya kutatua changamoto hizo.

Aidha, aliishauri serikali kushirikisha sekta binafsi ili kuja na suluhu ya changamoto ya nishati katika migodi na kuachana na matumizi ya mafuta katika kuendesha mitambo migodini.

Hata hivyo, amesisitiza kuhamasisha na kuvutia uwekezaji na matumizi ya nishati jadidifu na hasa uwekezaji wa umeme jua katika migodi yote na hasa ile ambayo bado haijaunganishwa na gridi ya taifa.