ACT-Wazalendo yashauri serikali inunue chakula

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeishauri serikali inunue na kuhifadhi chakula cha kutosha angalau miezi mitatu kutoka kwenye chakula kitachovunwa mwaka huu ili kuepuka upungufu wa chakula.

Waziri Kivuli wa Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Mtutura Abdallah Mtutura alitoa ushauri huo katika taarifa aliyoitoa kuhusu uchambuzi wa bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mtutura alieleza kuwa serikali itaweza kufanya hivyo kwa kuongeza bajeti kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inunue tani milioni 1.5 za mahindi, tani laki tano za mpunga na maharagwe tani milioni moja.

Chama hicho pia kimeishauri serikali iweke mazingira bora kwa wakulima wadogo ili waongeze uzalishaji zaidi kwa kuendelea kutoa ruzuku katika mbolea, kusimamia usambazaji na kuhakikisha usalama wa ardhi kwa wakulima wadogo kwa kushughulikia migogoro ya ardhi.

Kiliishauri serikali iwekeze nguvu zaidi kwenye mabonde ya mto Ruvu, Rufiji, Pangani, Kilombero, Ruvuma, Mbwenkuru, Ruaha, Kihansi, Mara na mabonde ya Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria.

Kilisema pia ni muhimu kuunganisha maendeleo ya viwanda na ukuaji wa kilimo na pia serikali iweke mkazo kwenye viwanda vidogo maeneo ya vijijini vinavyoendeshwa, kumilikiwa na kusimamiwa na wakulima wenyewe kupitia vyama vya ushirika.

“Aidha, mikakati ya kilimo lazima ifungamanishwe na viwanda ili kuongeza thamani, kuongeza uzalishaji na kuhakikisha kunakuwa na masoko ya uhakika wa bidhaa za mazao ndani ya nchi na zaida kusafirishwa nje,” alieleza Mtutura.

Chama hicho kiliishauri serikali iharakishe na kukamilisha kazi ya kupima, kurasimisha na kumilikisha ardhi kwa wananchi ili kuepusha migongano.

“Vilevile, mamlaka za halmashauri zijengewe uwezo stahiki na kuwezeshwa ipasavyo ili ziweze kushughulikia migogoro ya ardhi upesi na kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha ardhi imepimwa na kurasimishwa kwa wananchi,” alieleza Mtutura.

Habari Zifananazo

Back to top button