Aeleza mikakati kuendeleza sekta ya sheria

NAIBU Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Boniface Luhende

NAIBU Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Boniface Luhende amesema Serikali imeweka mikakati ya kuendeleza sekta ya sheria ili kuwahudumia wananchi vyema zaidi.

Akizungumza katika kikao kazi cha wakurugenzi na wakuu wa vitengo vya sheria wa kutoka wizara mbalimbali, taasisi za serikali, mashirika ya umma na halmashauri zote nchini, Dk Luhende alisema maendeleo ya taifa na wananchi yanategemea sana sekta ya sheria.

Alifafanua kwamba sekta hiyo ni nyezo muhimu katika maendeleo ya taifa na ndio maana serikali imekuja na mikakati ya kuendeleza sekta hiyo.

Advertisement

Dk Luhende alisema hata kufanyika kwa kikao hicho ambacho kimewakusanya viongozi hao ili kupanga mikakati ya kuendeleza sekta ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu ni sehemu ya mikakati ya kuendeleza sekta katika kupata wanasheria wabobezi ndani ya serikali.

Alisema kwa kufanya hivyo kunaisaidia serikali kutekeleza majukumu yake kulingana na kaulimbiu ya mwaka huu isemayo: ‘Utekelezaji wa Majukumu Unaozingatia Sheria ni Nyenzo Muhimu kwa Maendeleo ya Taifa’.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dk Eliezer Feleshi alisema ni muhimu kwa viongozi hao kuelewa dira na dhima ya ofisi wanazotumikia.

Alisema kwa kufanya hivyo kutawafanya waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha na ufanisi zaidi.

Dk Feleshi alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa mawakili wa serikali kuendelea kujisajili kwenye mfumo ili waweze kutambulika wasifu wao na kazi wanazofanya.

“Utumishi wa umma tunaoutaka kwenye sekta ya sheria ni kuhakikisha kuwa kila mtumishi wa umma wa kada ya sheria anatumika kutokana na uwezo wake mahali alipo.

“Anaweza kuwa mwajiriwa wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali lakini akatumika kufanya kazi kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwa siku hizi tunasoma kuwa mahiri na sio kusoma bora tu kusoma,” alisema.

Dk Feleshi alisema mpaka sasa mfumo wa taarifa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu unaonesha kuna mawakili wa serikali 2,661 wamesajiliwa ambapo kati ya hao mawakili 18 wana shahada ya uzamivu, 789 wana shahada ya uzamili, 863 wana astashahada ya juu na mawakili 855 wana shahada ya kwanza ya masuala ya sheria.

Naye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Shaban Ramadhan Abdallah, alisema kuwa wamekuja kujifunza ili nao waweze kuiga na kwenda kutekeleza mashirikiano hayo baina ya Ofisi hiyo ya SMZ na za Tanzania Bara.