Afrika yapania makubwa uzalishaji chanjo

MKURUGENZI Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (CDC AFRIKA) Dk Jean Kaseya amasema miongoni mwa dira ya Mkutano wa Tatu wa Afya ya Jamii(CPHIA 2023) unaoendelea Lusaka ,Zambia ni kujenga uwezo wa uzalishaji wa ndani ya Afrika wa chanjo zinazotumika Afrika kwa asilimia 60.
Ili kufanikisha hilo Dk Kaseya amesema Muungano wa Kimataifa wa Chanjo (GAVI) umetoa dola bilioni 1 kusaidia mataifa ya Afrika katika kuongeza uzalishaji wa chanjo, ikilenga kufikia asilimia 60 ya mahitaji ya chanjo ya ndani ifikapo 2040, kutoka asilimia 30 ya sasa.
“Ni asilimia moja tu ya chanjo zinazotumiwa barani Afrika zinazalishwa hapa na ni asilimia tano pekee ya uchunguzi unaotumika barani Afrika hutoka hapahapa, ambapo kati ya asilimia 25 na 30 pekee ya dawa zinazotumiwa barani Afrika zinatoka Afrika hivyo tunatakiwa kukomesha,” alisisitiza Dk Kaseye.

Amesema serikali za Afrika zinapaswa kuunda ushirikiano ili kutengeneza chanjo na kufanya mifumo yao ya afya kuwa thabiti ambapo , ni sehemu muhimu ya maandalizi ya bara kwa janga la siku zijazo.
“Uwezo huu mdogo wa uzalishaji umeifanya Afrika kutegemea kwa kiasi kikubwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje, na hivyo kuzidisha tofauti za kiafya na kuzuia upatikanaji wa chanjo za kuokoa maisha hali inayoathiri maisha ya watu wengi,” amesema.
Kwa Upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Dk Pauli Kzyoba, amesema mkutano huo umebeba ajenda kubwa kwani matumizi ya dawa kwa Afrika yanatumia fedha nyingi, hivyo kukiwa na uzalishaji wa chanjo na dawa itapunguza gharama.
“Kwanza zitazalisha ajira kwa vijana mamilioni na pia upatikanaji wa chanjo na dawa utakuwa rahisi na kuna ajenda ya ununuzi wa dawa kwa pamoja kama inavyofanywa na global Fund kwasababu watu wa viwanda nchi mmoja mmoja inaenda na oda ndogo lakini tukiunganisha bajeti zetu inakuwa na nguvu kubwa,”ameeleza Dk Kazyoba.
Maofisa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) na wawakilishi wa serikali kutoka bara zima walisema ipo haja ya Afrika kuweza kutengeneza chanjo yake yenyewe, na wametaka ushirikiano na uwekezaji ili kufanikisha hili.

Katika Mkutano huo zaidi ya wajumbe 5,000 kutoka kote barani Afrika na kwingineko wamekusanyika kujadili maendeleo yaliyopatikana katika mwaka uliopita wa Mkutano uliofanyika Kigali Rwanda ambapo kauli mbiu ni “Kuvunja Vizuizi: Kuweka upya Afrika katika Usanifu wa Afya Ulimwenguni.



