Agizo la Tanga ya viwanda laanza kutekelezwa

TIMU ya ufuatiliaji iliyoundwa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara imekutana na wadau wa sekta ya viwanda mkoani Tanga, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuirejesha Tanga ya viwanda.

Akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga hivi karibuni, Rais Samia alisema miongoni mwa ndoto zake katika kuiongoza Tanzania ni kuirejesha Tanga kuwa mkoa wa viwanda kama ilivyokuwa awali.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda na Biashara, Juma Mwambapa alisema juhudi za kuirejesha Tanga ya viwanda ni sehemu ya mkakati wa serikali katika kuimarisha uchumi wa viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Advertisement

“Tanga inakwenda kuwa kitovu cha viwanda nchini hivyo kwa kushirikiana na wadau wote muhimu tunakwenda kurudisha hayo na hivyo kufungua fursa za ajira, lakini na kuimarisha uchumi wa mkoa huu,” alisema Mwambapa.

Aidha, alisema kuimarika kwa miundombinu muhimu kama bandari, reli na barabara kuna kwenda kutoa fursa ya kuimarika kwa uchumi wa viwanda kwenye mkoa huo.

“Tunakutana na wadau ili kuweza kubaini changamoto zilizosababisha viwanda kufa lakini na kuweka mazingira rafiki ya kufanikisha uwekezaji wa viwanda hivyo lakini na kufufua vilivyokuwepo hapo awali,” alibainisha.

Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Sebastian Masanja alisema uongozi wa mkoa huo upo tayari kushirikiana na wawekezaji katika kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanapatikana ikiwamo kutatua changamoto za miundombinu na malighafi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa TCCIA mkoani Tanga, Rashid Mwanyoka alisema wao kama wadau wakuu wa ajenda hiyo wameiomba serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwamo kubainisha maeneo mahususi kwa ajili ya fursa za uwekezaji huo wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *