Akaribisha kampuni za bima za India kuwekeza

BALOZI wa India nchini , Binaya Pradhan amezitaka kampuni zinazotoa huduma za bima kuwekeza Tanzania, kwa kuwa kuna fursa nyingi na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Akizungumza katika mkutano uliokutanisha kampuni na taasisi za bima Tanzania na India jana Dar es Salaam, Pradhan alisema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imewahakikishia wawekezaji wote mazingira mazuri hivyo ni wakati wao kutumia fursa hizo Watanzania wanufaike na bima zinazotolewa.

Alisema wameandaa mkutano huo mahususi kubadilishana uzoefu wa namna ya kuendesha taasisi na kampuni za bima kwa sababu ni sekta yenye soko kubwa na la manufaa.

Alisema sekta binafsi ni kiungo muhimu kwa maendeleo ya nchi katika kukuza uchumi na kwamba soko la bima lina fursa nyingi ambazo zinahitaji wawekezaji.

Mkurugenzi Usimamizi wa Soko kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Abubakari Mgata alisema wanaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji wengi nchini na kwamba kampuni hizo zikiwekeza Tanzania zitasaidia upatikanaji wa ajira.

Alisema wanakaribisha kampuni hizo na nyingine kuwekeza Tanzania kwani tasnia hiyo inazidi kukua kwa sababu hadi mwaka jana, ada zilizolipwa ni zaidi ya Sh trilioni moja na kwamba wanakaribia nchi nyingine za Afrika zilizokua katika eneo hilo kama vile Morocco.

Mgata alisema sekta ya bima nchini bado ni changa, hivyo wameweka mikakati ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, asilimia 80 ya Watanzania wawe na uelewa kuhusu bima zinazotolewa ikiwamo za magari, maisha na afya.

Mwenyekiti wa Shirika la Bima ya Maisha India (LIC), Kumar Mangalam alisema kuwa wamekuja nchini kwa ajili ya kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta ya bima ili Watanzania wawe miongoni mwa nchi zinazonufaika na bima wanazozitoa.

Habari Zifananazo

Back to top button