KIGOMA: MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amewataka wasimamizi na watekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Kigoma kuhakikisha miradi hiyo inakamilika na wananchi wanapata huduma badala ya kuandika taarifa za kusifia wakati wananchi hawapati huduma.
Andengenye amesema hayo alipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa maji katika Kijiji cha Chakuru Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ambapo alikagua ukarabati wa tanki la kuhifadhia maji na utandazaji mabomba kwa ajili ya kwenda kwa wananchi.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa haiingii akilini wasimamizi wa miradi wanaposoma taarifa nzuri kwa viongozi wanaotembelea miradi wakionyesha miradi imetekelezwa vizuri wakati huduma hazipatikani kwa wananchi jambo ambalo amesema kuwa halikubaliki.
Awali akitoa taarifa kwa Mkuu huyo wa mkoa, Meneja wa Wakala wa maji mijini na vijijini (RUWASA) Wilaya ya Uvinza, Mhandisi Bakari Kiwitu amesema kuwa serikali imetoa kiasi cha Sh milioni 902.8 kwa ajili ya ujenzi wa tanki jipya la lita 140,000 na kukarabati la zamani la lita 40,000 na kilometa 16 za mtandao wa mabomba.
Mhandisi Kiwitu amesema kuwa kwa hatua za awali RUWASA inakarabati tanki la zamani la lita 40,000 na utandazaji mabomba mradi unaotarajia kuchukua wiki mbili kukamilika na kwamba kila kitu kipo eneo la mradi na kwamba utekelezaji wa mpango huo utakamilika kama ulivyoelezwa.
Akizungumza katika ukaguzi wa mradi huo Diwani wa Kata ya Uvinza, Aloka Mashaka amlishukuru Mkuu wa mkoa Kigoma kwa maelekezo hayo.