Argentina yatangulia nusu fainali Copa America

Nahodha wa Argentina, Lionel Messi(kulia) akishangalia pamoja na mchezaji mwenzake(Picha:https://sportstar.thehindu.com/)

MABINGWA watetezi wa Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini, Argentina imetinga nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuitoa Ecuador katika robo fainali kwa penalti 4-2.

Ushindi huo umeipa bingwa huyo mtetezi nafasi ya nusu fainali mashindano hayo kwa mara ya tano mfululizo licha ya nahodha Lionel Messi kukosa penalti ya kwanza.

Golikipa wa Argentina, Emi Martinez.(Picha: MailOnline)

Golikipa Emi Martinez alikumia mkombozi wa Argentina katika ushindi wakati mlinda mlango huyo alipookoa mabao mawili muhimu na kuiweka timu yake katika nafasi nzuri baada ya Messi kukosa penalti.

Advertisement

Hadi muda wa kawaida wa dakika 90 timu hizo zilikuwa sare ya 1-1 wakati wa mchezo huo uliofanyika uwanja wa NRG uliopo jiji la Houston, Jimbo la Texas, Marekani.

“Niliwaambia vijana kuwa sikuwa tayari kurudi nyumbani. Wao pia hawakuwa,” alisema golikipa Martinez baada ya kutajwa kuwa mchezaji bora wa Mechi.

Soma: http://Argentina yaanza vyema kutetea taji la Copa America

Kufuatia kipigo hicho, Ecuador imemfuta kazi kocha mkuu Felix Sanchez.

“Tunamshukuru Felix na jopo lake la ufundi kwa kazi yao na weledi wao, na tunamtakia mafanikio katika jitihada zake zijazo,” Shirikisho la Mpira wa Miguu Ecuador (FEF) limeeleza.

Argentina itakutana na Canada au Venezuela katika nusu fainali huku ikitafuta kushinda taji la 6 la Copa America.

Copa America ni moja ya mashindano ya soka ya zamani na yenye hadhi kubwa duniani, yanayoshirikisha timu za mataifa ya Amerika Kusini.

Yakiandaliwa na Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (CONMEBOL), mashindano hayo yana historia ndefu inayorudi hadi mwaka 1916.

Hapo awali yalifanyika kusherehekea miaka mia moja ya uhuru wa Argentina na muundo wake umepitia mabadiliko mbalimbali.

Copa America imekuwa jukwaa kwa wanasoka maarufu kuonyesha ujuzi wao wakiwemo wakongwe kama Diego Maradona, Pelé, na hata Lionel Messi wote wamecheza kwenye mashindano haya, wakiacha alama isiyofutika kwenye urithi wake.

Moja ya sifa za kipekee za Copa America ni ushindani wake mkali.

Mechi kati ya nchi jirani kama Brazil na Argentina, Uruguay na Argentina, au Chile na Peru ni matukio yenye hisia kali yanayovutia mashabiki kote barani Amerika Kusini.

Katika miaka ya hivi karibuni, Copa America imeendelea kukua katika hadhi na mvuto wa kimataifa.

Kwa kushirikisha timu za mwaliko na ushiriki wa wachezaji wa daraja la dunia, mashindano haya yanavutia watazamaji wa kimataifa, na kuyafanya kuwa tukio kuu la soka la kimataifa.