Ashauri mbinu zitafutwe maskini kuchangia uchumi

SERIKALI imeshauriwa kutumia takwimu za pato ghafi la nchi kuweka uwiano wa vipato katika sera za kiuchumi ili kupunguza pengo la masikini na matajiri.

Profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Deo Kinyondo amesema haitoshi kupima maendeleo ya uchumi kwa kutumia takwimu za pato ghafi kwa kuwa hakuna uhalisia katika maisha ya wananchi wengi.

Profesa Kinyondo alisema wananchi wanalalamika kuwa wana hali ngumu ya maisha wakati serikali inasema uchumi unakua kwa sababu kuna uwezekano watu wachache au sekta chache zinachangia ukuaji huo, hivyo kundi kubwa likabaki masikini.

Wakati akizungumza katika kipindi cha Morning Express cha kituo cha redio cha UFM alisema pato ghafi la nchi ni jumla ya thamani ya mapato yote ya uzalishaji ya nchi husika katika mwaka mmoja na akasema kigezo hicho kinazingatia jumla ya mapato na kusahau tofauti ya vipato vya wananchi kwenye nchi husika.

“Ni kweli haidanganyi uchumi umekua, ni kweli serikali haidanganyi kwamba mpaka sasa tupo katika uchumi wa kati wa chini, ni kweli kwamba tumepiga hatua lakini kwa kigezo ambacho sio jumuishi,” alisema.

Alihimiza serikali itumie takwimu hizo kutafuta namna ya kufanya uchumi huo uchangiwe na watu wengi wakiwamo masikini.

Profesa Kinyondo alisema kwa kuzingatia hili huenda sehemu kubwa ya mapato ghafi yanayotajwa yanamilikiwa na watu wachache tu kwenye nchi husika hivyo kundi kubwa linaendelea kuwa masikini.

“Kuna watu ambao siku zote uchumi wao unaweza usikue au unaweza ukawa umeshuka lakini bado uchumi mpana huu tunaouzungumzia ukawa umekua kwa sababu tofauti za kipato haziwekwi katika kuhesabu pato la taifa kwa maana ya GDP, ndio maana kunakuwa na tatizo watu wanasema mnatudanganya, hiyo ipo kwenye makaratasi tu,” alisema profesa.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Lawi Yohana alisema ujenzi wa uchumi unapaswa kuwa shirikishi ili uakisi maisha ya wananchi wakiwamo maskini.

Dk Yohana alisema Mtanzania anaweza kujipima kupitia uchumi wake na kwamba serikali inafanya kazi kuwasaidia watu ambao hawajafikia kiwango hicho kwa kuwawezesha kupata mikopo na huduma za bure.

“Serikali ilianzisha Wakala wa Nishati Vijijini (REA) sera uliolenga kuwasaidia wananchi wa chini kuunganishwa na umeme kwa kuwa tayari wenye kipato cha juu wamechangia huduma hiyo, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), mikopo ya asilimia 10 kwa halmashauri yote inalenga kuwezesha makundi mbalimbali kuinua kipato chao,” alieleza.

Pia alisema sera ya elimu bure kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha sita, huduma ya matibabu bure kwa watoto chini ya miaka mitano na wazee zinalenga kuhakikisha watu wake wanaishi kulingana na viwango hivyo.

“Serikali haiwezi kugawa fedha inachogawa ni huduma za jamii, hivyo ukizijumuisha inakuwa imemsaidia mwananchi kufikia viwango lakini tunaomba iendelee kutoa ruzuku, huduma za jamii na mikopo ya wajasiriamali, huduma bure za afya kwa wazee na watoto na kuweka mazingira wezeshi ili kuwafanya wananchi waweze kukua kiuchumi,” alisema.

Mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi, Gabriel Mwang’onda alisema serikali inapigana kuhakikisha inapunguza nafasi kati ya walionacho na wasionacho hivyo Mtanzania binafsi hawezi kuona kama uchumi unakua.

Mwang’onda alisema uchumi umekua kwa sababu nyingi ikiwemo ongezeko la bajeti ya kutoka Sh trilioni 42 hadi Sh trilioni 48, inakusanya kodi kutoka wastani wa Sh trilioni 1.2 kwa mwezi wakati wa serikali ya awamu ya tano hadi Sh trilioni mbili zinatokana na ongezeko la uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

“Serikali inarudisha fedha kwa watu kwa njia ya huduma za kijamii kama vile utoaji wa elimu bure, matibabu ya wazee na watoto bure, ujenzi wa barabara, miradi mikubwa inaendelea. Huo ni ukuaji wa uchumi kwani walioajiriwa hata kama ni mama nitilie hapo wataona ukuaji wake tofauti na mtu ambaye hajishughulishi kwa lolote,” alieleza Mwang’onda.

Habari Zifananazo

Back to top button