Askari 4 mbaroni tuhuma mauaji ya mkulima Geita

JESHI la Polisi mkoa wa Geita linawashikilia askari wanne wa Jeshi la Uhifadhi kwa tuhuma za mauaji ya mkulima na mkazi wa kijiji cha Msonga wilayani Bukombe, Eziboni Fikiri (20).

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Adamu Maro amesema tukio hilo la mauaji limetokea Agosti 13, 2025 majira ya saa 12 asubuhi.

Amesema tukio lilitokea eneo la pori la hifadhi ya Kigosi wilayani humo wakati askari hao wakitekeleza jukumu la ukamataji watu waliokuwa wameingia hifadhini na kukata miti kinyume cha sheria.

Amesema askari hao wote wanashikiliwa kwa uchunguzi zaidi ili kubaini kwa kina kiini cha tukio hilo na kuruhusu vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za kinidhamu pamoja na sheria kufuata mkondo wake.

Amesema hadi kufikia Agosti 14, 2025 mwili wa marehemu ulikuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu.

Jeshi la Polisi linawaomba wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi wa tukio hilo unaoendelea kufanyika ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

“Watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo”, amesema Maro.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button