WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso ametaja vipaumbele vitano vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwamo kuendelea na utunzaji wa vyanzo vya maji ikihusisha kutambua na kuweka mipaka.
Aweso amesema hayo bungeni Dodoma jana wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Wizara imeliomba Bunge liidhinishe zaidi ya Sh bilioni 756.2 na kati ya hizo, Sh bilioni 695.83 ni za maendeleo. Sh bilioni 407 sawa na asilimia 58.50 ya bajeti hiyo ni fedha za ndani na Sh bilioni 288.765 sawa na asilimia 41.50 ni fedha za nje.
Aweso alisema mbali na kulinda na kuvitangaza vyanzo vya maji kwenye Gazeti la Serikali, pia kuimarisha usimamizi wa ubora wa maji.
Aweso alisema kipaumbele kingine ni kukamilisha ujenzi na ukarabati na upanuzi wa miradi inayoendelea kutekelezwa ikiwemo miradi ya maji katika miji 28.
Alisema pia kuendelea na ujenzi wa bwawa la kimkakati la Kidunda na kuanza ujenzi wa Bwawa la Farkwa na kusanifu na kutekeleza miradi ya maji kwa kutumia vyanzo vya uhakika ikiwemo maziwa makuu na mito mikubwa ili kuyapeleka maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji.
Akizungumzia mpango wa utekelezaji, alisema mpango wa utekelezaji wa wizara kwa mwaka 2023/24 umeshirikisha wadau mbalimbali wakiwamo wabunge na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kuibua miradi ya kipaumbele.
Alisema mpango pia umejikita katika maeneo ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji ambapo katika mwaka 2023/24, jumla ya vyanzo 84 vitawekewa mipaka na kutangazwa kama maeneo tengefu.
“Pia serikali itafanya ukaguzi wa miundombinu ya utupaji majitaka katika migodi, viwanda pamoja na maeneo mengine,” alisema Aweso na kufafanua kuwa katika ujenzi wa mabwawa, pia serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa uvunaji maji ya mvua na kuanza utekelezaji wa ujenzi wa bwawa moja kwa kila wilaya yenye mazingira yanayofaa kwa ujenzi huo.
“Pia kuongeza kasi ya ujenzi wa mabwawa ya maji ya ukubwa wa kati hususani katika maeneo yenye ukame na kujenga mabwawa ya kimkakati,” alibainisha.
Alisema pia usimamizi wa ubora wa maji na huduma za usambazaji majisafi na usafi wa mazingira vijijini na kuimarisha huduma za usambazaji majisafi na usafi wa mazingira mijini.
Aidha, alisema katika mwaka 2023/24, serikali imepanga kujenga mabwawa 27 ya ukubwa wa kati na kufanya upembuzi yakinifu kwa ukarabati na ujenzi wa mabwawa ya ukubwa wa kati kwa ajili ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua.
Kuhusu usimamizi wa rasilimali za maji, alisema wizara itakarabati vituo 135 na kujenga vituo 51 vya kufuatilia mwenendo wa rasilimali za maji, kutoa vibali 450 vya matumizi ya maji, kutoa vibali 30 vya kutupa majitaka, kuunda jumuiya 10 za watumia maji pamoja na kuzijengea uwezo jumuiya 87 na kuunda kamati tisa za vidakio.
Alisema pia wizara itaendelea kusimamia shughuli za uchimbaji wa visima vya maji, kuendesha majukwaa na vikundi kazi vya wadau wa sekta mtambuka wa rasilimali za maji na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za majishirikishi.
“Pia kuimarisha taasisi zinazosimamia rasilimali za maji nchini na kufanya tathmini ya thamani ya maji kiuchumi.”
Kuhusu usimamizi wa ubora wa maji, Aweso alisema wizara itaendelea kuimarisha uhakiki na ufuatiliaji wa ubora wa maji katika vyanzo vya maji 2,091; skimu 4,600 za usambazaji maji mijini na vijijini pamoja na mifumo 150 ya majitaka na kuziwezesha maabara tano kupata ithibati.
Pia kuhakiki ubora wa madawa ya kusafisha na kutibu maji kabla ya manunuzi na wakati wa matumizi, kuwezesha uandaaji na utekelezaji wa Mipango ya Usalama wa Maji inayohimili mabadiliko ya tabianchi kwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira 34 na Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii 100.
Alisema pia kutoa elimu kuhusu viwango vya ubora wa maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali na kuendelea kuimarisha maabara za ubora wa maji kwa kuzipatia vitendea kazi pamoja na kujenga na kukarabati majengo ya maabara.