Baa, klabu ‘zilizopigwa kofuli’ kufunguliwa ikiwa…

SERIKALI imeanza kuzifungulia baa na kumbi za starehe ambazo zimekidhi matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 ambayo pamoja na mambo mengine, imeweka kiwango cha mitetemo ya sauti.

Kwa Mujibu wa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo, hadi kufikia leo, Jumanne, kumbi baa tano zilizofungiwa jijini Dodoma zimeshafunguliwa na tayari nne zimeshaanza kazi baada ya kukidhi matakwa ya Sheria hiyo.

Dk Jafo amelazimika kutoa maelezo hayo Bungeni, Dodoma leo asubuhi baada ya Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ kuomba mwongozo kupitia Kanuni ya 54(1) akieleza kuwa taifa linakosa mapato kwa kufungwa kwa maeneo hayo.

Aidha, Musukuma amesema Watanzania wanashauriwa kupata muda wa kujiburudisha na si kujifungia ndani.
Baada ya kumsikiliza, Naibu Spika Musa Azan ‘Zungu’ alimtaka Dk Jafo kuelezea suala hilo.

“Kulikuwa na malalamiko…watoto wanapoteza usikivu, wagonjwa wanapoteza maisha. Hatujui ni akina mama wangapi wamepoteza ujauzito kutokana na kelele.

“Wengi wameanza ku-comply [kukidhi matakwa ya Kisheria] baa zote zitafunguliwa. Tumeweka utaratibu mzuri,” Waziri ameliambia Bunge.

Amesema kuwa baadhi ya watoa huduma wameanza kufunga vizuia sauti na kuandika barua, jambo ambalo limewafanya kufunguliwa biashara zao.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Sehemu ya 147 inaelekeza kuwa Kamati ya Taifa ya Viwango vya Mazingira (a) itabainisha taratibu kuhusu vipimo na uchunguzi wa uchafuzi kwa kelele na mitikisiko;

(b) itaweka viwango vya chini kuhusu utoaji uchafuzi kwa kelele na mitikisiko kwenye mazingira;

(c) itaweka vigezo na taratibu kuhusu vipimo vya uchafuzi kwa kelele na mtikisiko kutoka vyanzo vilivyopo na vya siku zijazo;

(d) itabainisha miongozo kuhusu uondoaji kelele zisizo na maana au mtikisiko unaofanyika kwenye mazingira;

(e) itaweka viwango vya chini vya utoaji wa kelele na mtikisiko vinavyofaa kwenye maeneo ya ujenzi, mitambo, magari, vyombo vya anga pamoja na vipaza sauti, na kwenye shughuli za kiviwanda na kibiashara;

(f) itachukua hatua madhubuti kuhusu uondoaji na udhibiti wa kelele kutoka kwenye vyanzo vilivotajwa kwenye aya (e); na (g) itapima viwango vya kelele inayotoka kwenye vyanzo vilivyotajwa kwenye aya (e).

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x