Bahemu mgombea ubunge CCM Ngara

BUKOBA : MGOMBEA Ubunge Ngara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dotto Bahemu ameibuka kuwa mgombea pekee katika Jimbo la Ngara baada ya Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kushindwa kurejesha fomu na vyama vingine kutochukua fomu ya kugombea katika nafasi hiyo.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ngara, Constantino Msemwa wakati akizungumza na HabariLEO amesema waliochukua fomu ya kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo hilo ni wawili ambao ni Bahemu kutoka CCM na Peter Ruzige kutoka Chaumma lakini mpaka wakati wa kufungwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu aliyerudisha ni Bahemu pekee.
Alisema Bahemu ametimiza vigezo vyote vinavyotakiwa kujazwa kwenye fomu, hivyo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imemteua kuwa mgombea wa nafasi ya ubunge Ngara. Naye Mgombea ubunge Muleba Kaskazini kupitia CCM, Adonis Bitegeko ni mgombea pekee katika jimbo hilo baada ya Chaumma kushindwa kurejesha fomu.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Muleba Kaskazini na Kusini, Yona Charugamba akizungumza na HabariLEO jana, alisema Wilaya ya Muleba ina majimbo mawili ya uchaguzi ambayo ni Muleba Kaskazini na Muleba Kusini ambapo Muleba Kusini ina kata 25 na Kaskazini ina kata 18. SOMA: Ndoinyo apitishwa, mwingine akiuka kanuni
Katika Jimbo la Muleba Kaskazini wagombea waliochukua fomu ni Adonis Bitegeko kutoka CCM na Eradius Kaitila ambapo mpaka wakati wa kufunga uchukuaji wa fomu alirejesha Bitegeko pekee. Kwa upande wa Jimbo la Muleba Kusini, vyama vitano vimejitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya ubunge ambavyo ni CCM, NCCR Mageuzi, TLP, ACT Wazalendo na Chaumma ambapo wagombea kutoka vyama hivyo ni Oscar Kikoyo (CCM), Benezeti Josephat (NCCR Mageuzi), Abihudi Mbekomize (TLP), Jonepo Rwakalela (ACT Wazalendo) na Khamis Yusuph wa Chaumma.



