Bajeti ya elimu juu 40% miaka mitano

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameeleza mafanikio ya sekta ya elimu, ikiwemo ongezeko la bajeti ya wizara hiyo kwa asilimia 40 kutoka mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026. Amesema chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, serikali imeongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu kutoka Sh bilioni 464 hadi bilioni 916.7 zinazotolewa katika vyuo vikuu na vyuo vya kati.
Amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi mkoani Dar es Salaam juzi. Profesa Mkenda amesema Serikali ya Awamu ya Sita inajivunia kuongezeka uwekezaji katika miundombinu ya kujifunzia. Amesema wizara imejipanga kutekeleza ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100 ya kuhakikisha wanafunzi wa darasa la tatu wanamudu kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) unaotarajiwa kuzinduliwa mwezi Januari.
Kuhusu changamoto ya wanafunzi wengi kuacha shule, Profesa Mkenda alisema changamoto hiyo si ndogo na tayari wizara ilibainisha chanzo kimojawapo ni changamoto za kifamilia na baadhi ya wanafunzi kujiingiza kwenye shughuli za kiuchumi kama madini na ufugaji. Amesema moja ya suluhisho kwa changamoto hiyo ni kuandaa mfumo unganishi kwa wanafunzi unaotumia namba, utakaowezesha mwanafunzi kuwa na namba moja kuanzia anaanza shule ya msingi hadi anapomaliza chuo kikuu.
Profesa Mkenda amesema kuhusu wanafunzi wa madarasa mawili watakaomaliza mwaka mmoja, zipo njia za kuwatosheleza kumaliza na kuwa wengine wataenda sekondari, shule za amali huku wengine watapelekwa kupata mafunzo ya ufundi na ufundi stadi.
Amefafanua juu ya lugha ya kufundishia shuleni, Profesa Mkenda alisema kwa shule ya msingi lugha itakayotumika kufundishia ni Kiswahili na Kiingereza litakuwa somo, wakati sekondari lugha itakayotumika ni Kiingereza na Kiswahili litakuwa somo. “Kama unataka kufundisha mtaala wa Kiingereza kwa shule ya msingi, utaomba kibali maalumu na lazima ufundishe Kiswahili kuanzia darasa la kwanza na kama unataka kufundisha mtaala wa Kiswahili, utaomba kibali maalumu na Kiingereza litakuwa somo.Hatuwezi sisi tukaacha kufundisha kabisa Kiswahili moja kwa moja,” alisema.
Amesema mfumo huo ukikamilika, kuna uwezekano wa shule za sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne zikafundisha kwa lugha ya Kiswahili masomo yote. SOMA: Serikali yataka mikakati wanafunzi elimu ya juu tiba



