Bandari ya Mtwara yaandika historia
BANDARI ya Mtwara imepokea meli yenye urefu wa mita 240 ikiwa ni meli kubwa zaidi kuwahi kutia nanga katika historia ya bandari hiyo.
Meli hiyo ya MV GH Tranmotane imetia nanga leo iikiwa na makontena 459 kwa ajili ya kusafirisha korosho ghafi kwenda mataifa mbalimbali duniani.
SOMA: Bandari ya Mtwara kufungua zaidi mauzo ya Korosho
Akizungumzia ujio wa meli hiyo Mkuu wa Kitengo cha Ubaharia Bandari ya Mtwara, Kapteni Paul Mchawampaka amesema meli hiyo imeweza kutia nanga Mtwara kutokana na ufanisi na teknolojia ya kuhudumia meli kubwa zaidi.
“Bandari ya Mtwara ilitengenezwa kwa ajili ya kuhudumia meli zenye urefu wa mita 176 tu lakini kutokana na ongezeko la teknolojia na namna ambavyo kumekuwepo na maboresho na ushindani wa biashara tumeweza kupata meli hii kubwa bandari ya Mtwara,” amesema.
Amesema kutokana na ujio wa meli hiyo, Bandari hiyo imevunja rekodi ya kuingiza meli yenye mita 240.
Meneja wa Bandari hiyo Ferdinand Nyathi amesema meli hiyo imeleta kontana ambazo zitatumika kuhudumia korosho ghafi kwa msimu wa 2024/2025 ambao unatarajia kuanza Oktoba 11.
“Ujio wa meli hii ni kiasharia cha kufungua msimu mpya wa kusafirisha korosho kwa mwaka 2024/2025, na mwaka huu kuna mabadiliko makubwa, tumepokea makontana mapema kwa ajili ya maandalizi kusaifirisha korosho kwa ufanisi,” amesema.