MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imesema Bandari ya Mtwara imejipanga kusafirisha korosho ghafi ambazo zinatarajiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi msimu wa 2024/2025.
Taarifa hiyo imetolewa leo Oktoba 26, na Meneja wa Bandari ya Mtwara, Fernand Nyathi ambapo amesema bandari hiyo imejiandaa vya kutosha kuhudumia shehena yote ya korosho kadri zitakavyokuja.
Meneja huyo ameongeza kuwa idadi ya vifaa vya vyote muhimu vya kuhudumia shehena ikiwemo ‘Mobile Cranes’ vimeongezeka na kuleta ufanisi katika kuhudumia mizigo bandarini.
‘Licha ya kuwa na vifaa vyote muhimu, makasha (makontana) ya kubebea korosho hizo yalianza kufika mapema kabisa kabla ya msimu wa mauzo ya korosho,’ amesema na kuongeza kuwa mpaka sasa bandari hiyo imepokea makontana tupu 3700 kwa ajili ya kuhudumia korosho za kusafisha kwenda nje,” ameongeza Fernand Nyathi.
Makontana hayo kwa mujibu wa Nyathi yaliletwa na meli saba tofauti kuanzia Septemba 19 mwaka huu. Amesema meli nyingine tatu zinatarajiwa kuingia bandarini hapo kuleta makontana na kupakia mzigo wa korosho ghafi.
SOMA: Bandari ya Mtwara yaandika historia
Mwaka Jana (Msimu wa 2023/2025) bandari hiyo ilisafirisha korosho tani 253,000 huku msimu huu wa 2024/2025 wakitarajia kusafirisha zaidi ya 300,000.
Bodi ya korosho nchini (CBT) imesema zaidi ya tani 500,000 zinatarajiwa kuzalishwa msimu huu wa 2024/2025 kutoka 310,787 zilizozalishwa 2023/2024.
Nyathi amesema hatua hiyo ni kufuatia agizo la Raisi Samia Suluhu kuhakikisha korosho zote zinazotakiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi kutoka mikoa ya kusini zinasafrishwa kupitia Bandari ya Mtwara.