Bashe: Mabadiliko ya tabianchi kihatarishi kwa Taifa

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kihatarishi namba moja kwa taifa hivi sasa itakuwa ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha kupungua kwa uzalishaji wa chakula na hivyo kuhatarisha uimara wa uchumi wetu na usalama wa Taifa letu.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/24, amesema: “Ili kuwa salama kwenye eneo hili ni lazima kuendelea kuwekeza katika mifumo imara na himilivu ya kilimo inayotumia teknolojia za umwagiliaji za kisasa,uwezo wa kuhifadhi mbegu zetu za asili ili kuwa msingi imara wa kufanya utafiti kupata teknolojia bora za uzalishaji wa mbegu ili kujihakikishia usalama wa chakula na ulinzi wa uchumi wetu.

“Taifa lolote ambalo liko huru, lenye kulinda heshima na utu wa watu wake, ni lile ambalo linajitosheleza kwa chakula na uchumi imara.

“Ili uwe na uhakika wa chakula ni lazima kuimarisha uzalishaji, tija na kuwa na umiliki wa mbegu zetu kwani atakayetawala dunia hii ni yule ambaye ana umiliki wa mbegu bora na utoshelevu wa chakula.

“Tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe imebaini kuwa na upungufu wa uzalishaji katika baadhi ya maeneo katika msimu wa 2021/2022 uliotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na hivyo kusababisha kupanda bei kwa baadhi ya mazao ya chakula.

“Ili kukabiliana na hali hiyo, Wizara kupitia NFRA ilichukua hatua za kusambaza chakula 12 wastani wa tani 75,282.30 za mahindi na kuuzwa kwa bei ya chini ya soko kati ya Shilingi 680 hadi 920 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya soko ya Shilingi 1,200 hadi 1,500 lengo likiwa ni kumlinda mlaji na kudhibiti mfumuko wa bei,” amesema Waziri Bashe na kuongeza:

“Ili kukabiliana na upungufu wa chakula, Serikali inaendelea kuongeza uwezo wake wa kuhifadhi chakula kutoka tani 251,000 za sasa hadi tani 506,000.

“Aidha, kwa sasa Serikali imeanza shughuli ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujenga miundombinu ya uhifadhi itakayoongeza uwezo wa kuhifadhi kufikia tani 3,000,000 ifikapo mwaka 2030.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa, Taifa letu linauwezo wa kuhifadhi chakula cha kutumia miezi sita (6) pindi inapotokea janga ili kulinda uchumi wetu, heshima yetu, utu wetu na uhuru wetu,” amesema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button