Bil 100/- kuanzisha ujenzi vyuo vya Veta 62

SERIKALI imetenga Sh bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika wilaya 62, ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo vya ufundi stadi.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Mashariki, Dk Pius Chanya (CCM) aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kujenga chuo cha Veta wilayani Manyoni.

Profesa Mkenda alisema serikali inayo azma ya kujenga chuo cha ufundi stadi katika kila mkoa na wilaya zote nchini na katika mwaka huu wa fedha 2022/23, imetenga kiasi hicho kwa ajili ya kuhakikisha vyuo vya Veta vinajengwa katika wilaya hizo zilizobaki ikiwamo ya Manyoni.

Hata hivyo, Mkenda alishauri wananchi wa Wilaya ya Manyoni wakiwemo wa Jimbo la Manyoni Mashariki kuendelea kutumia chuo cha ufundi stadi cha Mkoa wa Singida.

Pia wananchi hao wanaweza kutumia chuo cha Wilaya ya Ikungi pamoja na vyuo vya Singida na Msingi FDC na vyuo vingine vya ufundi stadi vilivyopo nchini.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge Chaya aliyetaka kujua serikali ina mkakati gani wa kuweka elimu ya ufundi kuwa ya msingi ili kila kijana anayehitimu kidato cha nne ambaye haendelei na masomo au aliyehitimu kidato cha sita haendelei na masomo awe na ujuzi wa ufundi wake, Profesa Mkenda alisema hivi sasa serikali inapitia mitaala ili kuongeza mambo mbalimbali ikiwemo elimu ya ufundi na rasimu hiyo itakamilika mwishoni mwa mwaka huu.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button