Bil 20/- kufikisha maji Bandari ya Kwala
WIZARA ya Maji imeridhia kutoa Sh bilioni 20 kwa ajili ya mradi wa maji katika bandari kavu ya Kwala iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Riziki Shemdoe alisema hayo jana baada ya ziara ya makatibu wakuu wa baadhi ya wizara kukagua kazi zinazoendelea kwenye eneo la bandari hiyo.
Ujenzi wa bandari hiyo na uendelezaji wa bandari zilizopo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.
Ilani inaielekeza serikali kuendeleza miundombinu ya uchukuzi zikiwamo bandari zote kwa kuwa ni hitaji la msingi katika kuchochea na kuwezesha maendeleo ya sekta za kiuchumi na kijamii.
Pia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) unaeleza umuhimu wa kuendeleza bandari zilizopo nchini zikiwamo bandari kuu tatu za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na bandari ndogo za Kilwa, Mafia na Lindi. Pia bandari kubwa katika maziwa ambazo ni Mwanza, Kigoma na Itungi-Kyela.
Shemdoe alisema fedha hizo zitatumika kufikisha maji kwenye eneo hilo muhimu kwa viwanda.
“Wizara ya Maji tayari imeshatoa kibali cha matumizi ya fedha kiasi cha shilingi bilioni 20 zitakazopeleka maji kwenye eneo hilo la kibiashara la Kwala lengo kuhakikisha mradi huo unakuwa na miundombinu yote,” alisema.
Wakati wa ziara ya Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema eneo la bandari hiyo lina ukubwa wa hekta 502 na limeunganishwa kwa miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilometa 15.5 kutoka Kwala hadi Vigwaza pamoja na reli ya kisasa na reli ya zamani.
Profesa Mbarawa alisema ujenzi wa mradi huo utagharimu Sh bilioni 37.2.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Allan Kijazi alipongeza juhudi za ujenzi wa eneo hilo na akaagiza wataalamu kutoka wizara hizo kujiongeza katika kuboresha eneo hilo badala ya kufungwa na yaliyokuwa kwenye makabrasha.
Kijazi alisema eneo hilo litakuwa na shughuli nyingi za kiuchumi kwa kuwa na huduma za biashara na nyinginezo. Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Gabriel Migire aliuhakikishia msafara huo kwamba mradi utakamilika kama ilivyopangwa.
Katibu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba aliwapongeza wataalamu kutoka wizara hizo kwa kazi wanayoendelea kuitekeleza Kwala na anatarajia ujenzi utakamilika kama ilivyopangwa.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ally Gugu aliipongeza serikali kwa uwekezaji huo unaolenga kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.