Bil 233/- za Japan kuwezesha vijana kuwekeza

TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Afrika zitakazonufaika na fedha za Mfuko wa Kukuza Uwekezaji barani Afrika kutoka Serikali ya Japan zitakazotolewa kuanzia Machi mwakani.

Mwenyekiti wa timu ya Afrika ya Keizai Doyukai (Chama cha Watendaji Wakuu wa Mashirika Japan), Mutsuo Iwai alisema hayo wakati akizungumza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ofisini kwao Marunouchi, Chiyoda-ku, jijini Tokyo, Japan.

“Ifikapo Desemba mwaka huu, tutazindua kampuni ya kusimamia mfuko huu wa uwekezaji wenye manufaa barani Afrika na utekelezaji utaanza Machi, 2023. Tunataraji ifikapo Machi, 2024 tutakuwa tumetoa kiasi cha dola za Marekani milioni 100 (Sh bil 233/-) kwa kampuni za vijana wanaochipukia ili kuwajengea ubia, kujifunza teknolojia mpya na kubadilishana ujuzi,” alisema Iwai.

Alisema fedha hizo za uwekezaji kwenye mitaji zimelenga kukuza biashara ambazo zitatatua changamoto za kijamii zikiwamo sekta za afya, kilimo, nishati na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Utoaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida aliyoitoa Agosti 27, mwaka huu wakati akitoa hotuba kwenye Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) uliofanyika jijini Tunis nchini Tunisia.

Kishida alisema Japan imelenga kukuza uwekezaji, na safari hii wamelenga kuwainua vijana wanaoanzisha kampuni kuwapa fursa vijana wa Afrika na wa Japan kufanya kazi kwa karibu.

Keizai Doyukai ni taasisi binafsi iliyoanzishwa Aprili 30, 1946 yenye wanachama wapatao 1,500 ambao ni watendaji wakuu na wamiliki wa kampuni kubwa za Japan wanaojihusisha na utoaji suluhisho kwa masuala ya kisera yanayohusu maendeleo ya nchi yao na dunia kwa ujumla.

Majaliwa pia alikutana na wawakilishi wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Japan (KEIDANREN) ofisini kwao Otemachi, Chiyoda-ku jijini Tokyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Hajime Kawamura alimweleza namna shirikisho lao linavyojihusisha na miradi ya maji, barabara, nishati, mawasiliano, utengenezaji wa kemikali na ununuzi wa mazao.

Wawakilishi wa kamati hiyo wanaotoka kampuni za Sumitomo, Marubeni, Toshiba, Komatsu na Mitsubishi walimweleza Majaliwa nia ya kuwekeza kwenye miradi ya nishati, huduma za mawasiliano na tehama.

Keidanren ni jumuiya ya kiuchumi iliyoanzishwa Agosti 16, 1946 yenye wanachama 1,494 ambao ni wawakilishi wa kampuni za Kijapani, ina vyama 108 vya wenye viwanda na taasisi 47 za kiuchumi kutoka mikoa yote.

Majaliwa aliwaeleza wafanyabiashara wa makundi yote mawili kwamba Serikali ya Awamu ya Sita iko tayari kufanya kazi na wawekezaji.

“Utashi wa kisiasa wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, utulivu na amani vilivyopo nchini, hali nzuri ya hewa, ujenzi wa bandari, reli na barabara, umeme na maji unawahakikishia wawekezaji uhakika wa mitaji pindi mnapoamua kuwekeza nchini Tanzania,” alisema.

Aliwahamasisha waje nchini kuwekeza kwenye sekta ya utalii ikiwamo ujenzi wa hoteli za nyota tano na kuanzisha michezo ya majini kwenye fukwe za bahari Zanzibar na Bara, kilimo cha mashamba makubwa na ujenzi wa viwanda.

Majaliwa pia alikutana na Rais wa Taasisi ya Zimamoto ya Japan, Kamishna Akimoto Toshifumi na kujadiliana uwezekano wa taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa askari wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto nchini.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Collin
Collin
8 months ago

Sorry i don’t see the attachment of your project as there is any link that we can use to register our account

Back to top button
1
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x