Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo ameupongeza uongozi wa kiwanda cha sukari Kilombero mkoani Morogoro kwa uwekezaji mkubwa ambapo sasa kinafanyiwa upanuzi mkubwa kwa gharama ya sh. Bilioni 650.
Uwekezaji huo utaongeza uwezo wa uzalishaji wa sukari kutoka Tani 130,000 za sasa hadi Tani 270,000 na hivyo kuchangia kuondoa upungufu wa sukari hapa nchini.
Akizungumza leo alipotembelea kiwanda hicho, Waziri Jafo amekipongeza pia kiwanda hicho kwa kuchangia upatikanaji wa ajira hapa nchini.
“Kwa sasa kiwanda hiki kimeajiri wafanyakazi 4500 huku wakulima 11,000 wamewezeshwa na wanauza miwa yao kiwandani hapa na mapato yanayokwenda kwa wakulima hao ni wastani wa sh. bilioni 67 kwa mwaka.”amesema Dkt. Jafo.
Dkt. Jafo amewahakikisha wawekezaji wote hapa nchini kwamba serikali itaendelea kulinda uwekezaji wa viwanda vya aina mbalimbali kwa lengo kukuza uchumi na kulinda ajira za watanzania.