SERIKALI kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) imesaini mikataba 93 ya Sh bilioni 868.56 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya dharura ya barabara na madaraja iliyoathiriwa na mvua za El Nino na Kimbunga Hidaya.
Akizungumza leo Novemba 1, mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo jijini Dodoma, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewataka wakandarasi waliosaini mikataba hiyo kufanya kazi kwa weledi na kwamba serikali haitasita kumchukulia hatua mkandarasi atakayekwamisha utekelezaji.
Aidha, Bashungwa amewataka Watanzania kupuuza taarifa zinazoeleza kuwa utekelezaji wa miradi ya ujenzi imesimama ambapo ameeleza kuwa Serikali kupitia Tanroads inaendelea na ujenzi wa miradi 87 ya barabara yenye jumla ya kilometa 3,140.7, madaraja na viwanja vya ndege na tayari Sh bilioni 53.9 zimetolewa malipo ya awali kwa wakandarasi kuanza utekelezaji wa miradi ya ujenzi.
SOMA: Bashungwa: Tumejipanga kuifungua Dar es Salaam
“Hizi fedha bilioni 53.9 haijafika hata mwezi tumezipokea kutoka hazina kwa kazi nzuri ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ili kuanza utekelezaji wa miradi nane ya barabara, hata juzi nimetoka kumkabidhi Mkandarasi ujenzi wa barabara ya Kyerwa – Omurushaka (km 50) … halafu mnasema Tanroads ipo hoi, tuachane na hawa watu wanaotumika”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa asilimia 90 ya miradi iliyosainiwa itatekelezwa na wakandarasi wazawa ikiwa ni dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwainua na kuwajengea uwezo kupitia utekelezaji miradi.
Ameeleza kuwa mitakaba 93 iliyosainiwa itatekelezwa katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Kagera, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Singida, Songwe, Shinyanga, Tanga na Kigoma.
Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Mohamed Besta ameishukuru serikali kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo na kuahidi kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuzingatia viwango na kukamilika kwa wakati.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ameeleza kuwa miradi mbalimbali katika mkoa wa Dodoma inaendelea kutekelezwa kwa kasi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma na kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Msalato na kusisitiza hakuna kazi ya ujenzi iliyosimama.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani ameishukuru serikali kwa utekelezaji wa miradi ya dharura ya madaraja na barabara ambapo takribani Sh bilioni 13 zitatumika kujenga madaraja na makalvati ya kudumu katika jimbo lake na kuipongeza Tanroads kwa kuongeza mtandao wa barabara katika kipindi cha miaka minne kutoka kilometa 45 hadi 309 ambazo zimeendelea kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kufuatia za mvua El Nino na Kimbunga Hidaya zilizonyesha kuanzia Septemba 2023 hadi Mei 2024, barabara mbalimbali nchini ziliathirika na jumla ya kilometa 520, madaraja na makalvati 189 yalikatika na mengine kuharibika vibaya ambapo Serikali ilitoa fedha za awali Sh bilioni 130 kurejesha miundombinu hiyo.