Bilioni 100/-kununua nafaka kwa wakulima

BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) imetenga Sh bilioni 100 za kununua mazao ya nafaka yakiwamo mahindi na mchele katika mwaka wa fedha 2023/24.

Mwenyekiti wa CPB, Salum Awadh alisema hayo Mwanza katika mkutano na wadau wa kilimo Kanda ya Ziwa.

Awadhi alisema mjadala huo ulilenga kuongeza ushirikiano ili kuongeza tija ya kilimo biashara nchini kwa kuwa na soko la ukakika la nafaka na uongezeaji thamani mazao hayo kwa teknolojia ya kisasa.

Alisema bodi itanunua mazao kwa wingi kutoka kwa wakulima kisha kuyaongezea thamani na kuyauza sokoni hali itakayosaidia kuboresha mnyororo mzima wa kilimo nchini kuanzia mkulima anapokuwa kuwa shambani, sokoni hadi kwa mlaji kupata chakula bora.

Awadhi alisema lengo la CPB ni kuwa kitovu cha biashara ya mazao ya nafaka na mchanganyiko mfano mpunga, mahindi, mhogo, nanasi, na ngano ili kuwatengenezea soko wakulima.

“Tunataka kuwaunganisha wakulima na fursa, tutawajengea uwezo na wakati huo huo wakinufaika na miundombinu ya bodi ikiwemo ghala na viwanda,” alisema.

Awadhi alisema kwa sasa bodi inajumula ya viwanda saba vya kuchakata nafaka ikiwemo kile cha mkoani Mwanza chenye uwezo wa kuchakata tani 96 kwa siku.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Bishara CPB, Evans Mwanibingo alisema viwanda vyote saba vina uwezo wa kuchakata tani 445 kwa siku, hivyo akawaomba wakulima kuchangamkia fursa kwa kulima mazao ya nafaka yanayoitajika kama malighafi katika viwanda hivyo.

Alisema Sh bilioni 100 iliyotengwa itawezesha kununua jumula ya tani 115,000 katika mwaka wa fedha ujao.

Aliwaomba wananchi hususani vijana kuchangamkia ajira zitakazoletwa na ongezeko la uzalishaji wa viwanda hivyo ikiwemo uuzaji wa bidhaa mbalimbali za CPB kama mabarozi wa bodi hiyo.

Mkurugenzi wa kampuni ya Lilian ABC, Liliani Herbert aliiomba bodi kuwashika mkono kiteknolojia wawekezaji wazawa katika viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.

Habari Zifananazo

Back to top button