Bima afya kwa wote suluhu kwa wajawazito
SERIKALI imesema mswada wa Bima ya afya kwa wote utakapokamilishwa utakuwa suluhisho la kupunguza gharama za malipo kwa akina mama wanaojifungua kawaida na operesheni
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Godwin Mollel leo Februari 7, 203 Bungeni mjini Dodoma akijibu swali la Mbunge wa Temeke Doroth Kilave aliyeuliza je serikali ina mpango gani wa kupunguza gharma za malipo kwa akina mama wanaojifungua kawaida na wale wa operesheni?
Mswada wa bima ya afya kwa wote unatarajiwa kupelekwa bungeni kesho kutwa Alhamisi.
Kwa mujibu wa waraka wa Wizara ya Afya juu ufafanuzi wa Muswada huo, Kupitia Sheria inayopendekezwa, Waziri mwenye dhamana ya masuala ya afya kupitia Kanuni ataweka viwango vya uchangiaji kwa kuzingatia uhitaji wa huduma, gharama halisi za matibabu na uwezo wa wananchi kuchangia na mapendekezo yaliyopo yatategemea maoni ya wananchi na ridhaa ya mamlaka zingine.
Aidha, Kilave aliuliza swali la nyongeza ambalo alitaka kufahamu serikali ina mpango gani wa vifaa vya kujifungulia kwa wanawake ili kuondoa gharama za kununua vifaa hivyo ikiwemo pamba.
Akijibu swali hilo, Mollel amesema ni suala ni la kisera kuwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano hawatakiwi kulipishwa matibabu.
Amewaomba wakuu wa wilaya na mikoa kushirikiana na Wizara ya Afya kusimamia suala hilo.