BRELA yawapeleka yatima100 Dodoma kutembelea miradi ya maendeleo

DODOMA – Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umeonesha dhamira ya dhati katika kutekeleza wajibu wa kijamii kwa kudhamini ziara ya mafunzo kwa watoto yatima na wenye ulemavu 100 kutoka Kituo cha Kulelea Yatima cha Tulee Yatima Tanzania (TUYATA) kilichopo Magomeni Mwembechai, Dar es Salaam kwenda jijini Dodoma kwa kutumia reli ya kisasa (SGR).
Ziara hiyo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa wakati wa futari maalum katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kurudisha kwa jamii kutokana na sapoti wanayoipata kutoka kwa wananchi.
Kituo cha TUYATA, kilichopo Mtaa wa Kondoa, Magomeni, kinahudumia watoto wenye ulemavu 36, yatima 200 na wajane 60, kwa kuwapatia malezi, elimu na msaada wa kijamii.
Akizungumza kwa niaba ya BRELA, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Bi Joyce Mgaya alisema ziara hiyo inaonesha dhamira ya BRELA katika kusaidia makundi yenye uhitaji maalum.

“Mtendaji Mkuu wetu aliona ni jambo jema kuwapa watoto hawa fursa ya kutembelea makao makuu ya nchi na kujionea miradi ya maendeleo inayotekelezwa,” alisema Bi Mgaya.
Bi Mgaya alifafanua kuwa katika mwezi wa Ramadhani, BRELA ilitoa mchango wa zaidi ya shilingi milioni nne kwa ajili ya kusaidia kituo cha TUYATA na tangu wakati huo taasisi imeendelea kushirikiana nacho kwa karibu.
Mkurugenzi na Mwanzilishi wa kituo cha TUYATA, Bi Fauzia Jabir aliishukuru BRELA kwa kile alichokiita “msaada usiosahaulika”.
“BRELA imefanya jambo kubwa kwa kusimama na watoto hawa wahitaji,ziara hii itawafanya wajifunze vitu vingi zaidi,” alisema Bi Jabir.

Hata hivyo, alieleza kuwa licha ya mafanikio ya kielimu waliyonayo, kituo hicho kinakabiliwa na changamoto kubwa ya makazi kwa watoto yatima, na hivyo kuomba msaada wa ujenzi wa nyumba za makazi kwa watoto na wajane.
Mmoja wa walionufaika na kituo hicho ambaye pia ni msemaji wa TUYATA,Bi Ayman Jaffar Abubakar alisema kulea watoto kutoka mazingira mbalimbali si kazi rahisi lakini kwa neema ya Mungu, wanajitahidi kutoa malezi bora na kuwaelekeza katika njia sahihi.
“Watoto wengi wanaishi kwa walezi, hivyo ni changamoto kuwafuatilia kikamilifu. Tunaishukuru BRELA kwa kutuunga mkono na tunaomba waendelee kuwa nasi hadi tufikie malengo yetu,” alisema.

Aliongeza kuwa ziara hiyo imefungua macho kwa watoto hao na kuwapa motisha mpya ya kujitahidi zaidi katika masomo na maisha yao.
“Mji wa Dodoma ni msafi, wa kuvutia na ni alama ya mamlaka. Tumefurahia kuona miradi ya Serikali kwa macho yetu wenyewe. Kupitia BRELA, tumepata maarifa na matumaini mapya,” alihitimisha.
Ziara hiyo inatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa watoto na wajane hao, huku BRELA ikielezwa kuwa mfano bora wa taasisi zinazojali na kushiriki maendeleo ya jamii.