Carneiro kurejea Chelsea?

Unamkumbuka yule daktari wa zamani wa kikosi cha Chelsea, Eva Carneiro sasa amedokeza uwezekano wa kurejea Stamford Bridge baada ya kundi kubwa la mashabiki kumsihi arejee.

Carneiro alifanya kazi na West Ham kabla ya kujiunga na Chelsea mwaka 2009. Miaka miwili baadaye, alipandishwa cheo kufanya kazi pamoja na timu ya kwanza na meneja wa wakati huo Andre Villas-Boas. Aliendelea na jukumu lake chini ya makocha Roberto Di Matteo, Rafael Benitez na Jose Mourinho.

Hata hivyo, mambo yalianza kuwa tofauti mwaka 2015 baada ya Mourinho kumkosoa hadharani yeye na mwanafizikia, Jon Fearn kwa kushindwa kumtibu Eden Hazard.

Advertisement

Mwezi mmoja baada ya tukio hilo, Mourinho aliondolewa, lakini Carneiro aliondoka Chelsea na kuipeleka klabu hiyo mahakamani kabla ya kulipa paundi milioni 5 kutokana na kutimuliwa kwake.

Tangu alipoondoka Chelsea, Carneiro amekuwa akifanya kazi kama mtaalamu wa The Sports Medical Group huko London huku pia akiwa mshauri wa hospitali ya Qatar kabla ya Kombe la Dunia.

Kama dokezo lake la kurejea litafanikiwa atakuwa msaada mkubwa ndani ya klabu hiyo, kwa kuzingatia kuwa Chelsea kwa sasa inakabiliwa na majeruhi ambao ni
Ben Chilwell, N’Golo Kante, Ruben Loftus Cheek, Armando Broja, Wesley Fofana na Carney Chukwuemeka.

Kutokana na orodha yao ya majeruhi inayozidi kuongezeka, mashabiki wa Chelsea wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kumtaka Carneiro arejee katika klabu hiyo. Shabiki mmoja alichapisha picha ya daktari huyo yenye nukuu inayosema: “Ngoma ya mwisho?” Carneiro alijibu kwa: “Venga!”, ambayo inaweza kutafsiriwa kama “Njoo” au “Twende”.