CCBRT yaendesha huduma upimaji macho bure

HOSPITALI ya CCBRT iliyoko Msasani Dar es Salaam katika kuadhimisha Siku ya Afya ya Macho Duniani mwaka 2024, imeendesha huduma ya upimaji wa afya ya macho kwa wakazi wa Tegeta na maeneo ye jirani bila malipo.
Pia hospitali hiyo siku za hivi karibuni hospitali imefungua duka jipya la miwani katika jengo la Kibo Complex Tegeta, kwa lengo la kuwafikishia huduma hiyo muhimu wananchi wa maeneo hayo.
Kaulimbiu ya afya ya macho kwa mwaka huu inahimiza vijana na watoto kupenda macho yao na kuitaka dunia kuongeza umakini katika upatikanaji wa huduma bora za macho kwa vijana.
“Siku hii sio tu imetengwa kwa ajili kuhamasisha, bali pia inalenga kuwasaidia watu kuchukua hatua za dhati za kutunza afya ya macho yao.

“CCBRT inalenga kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya rika tofauti katika jamii yetu, kuhakikisha kila mtu anapata huduma muhimu za macho. Hii ndiyo sababu, katika maadhimisho haya, tunafanya uchunguzi wa macho bure wa siku mbili tarehe 9 na 10 Oktoba 2024 nje ya jengo Kibo Complex Tegeta, ambapo siku za hivi karibuni tumefungua duka jipya la miwani,” amesema Dk Cyprian Ntomoka, ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya macho kwa hospitali hiyo.
Isome pia:Presha ya macho kiini cha upofu
Amesema katika duka hilo wananchi wanweza kujipatia miwani kwa ajili ya matumizi ya kompyuta, simu, miwani ya jua, miwani ya kuendeshea gari na ile ya kusomea.
Amesema pamoja na matibabu ya magonjwa mengine, hospitali ya CCBRT kwa miaka zaidi ya 30 imekuwa kinara wa utoaji wa huduma bora za afya ya macho nchini.

“Kauli mbiu ya mwaka huu inatutaka wote tulinde afya ya macho yetu lakini imeenda mbali ikatutaka tulinde afya ya macho kwa watoto.
“Nitumie fursa hii kuwakumbusha tena wazazi na walezi wenzangu matumizi yasiyokuwa na mipaka ya vifaa vya elektroniki kama vile simu, kompyuta, televisheni na vingine vingi vyenye mwanga mkali vinaweza kuhatarisha afya ya macho ya watoto wetu.
“Nasisitiza umuhimu wa kulinda macho ya watoto ili kuzuia matatizo ya kuona yatokanayo na matumizi ya vifaa hivi,” ameonya Dk Ntomoka.



