CCM Tanga wageukia shule zake

Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Tanga, kimejipanga kuboresha miradi ya jumuiya ya wazazi iliyopo katika sekta ya elimu ambayo imeshindwa kufanya vizuri kutoka na uchakavu wa majengo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdulrahman wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya chama hicho sambamba na kusikiliza kero za wananchi katika Wilaya ya Handeni.
Amesema kuwa kama viongozi wa Chama lazima wakiri kuwa kuna mahali walikosea mpaka miradi hiyo Iliyokuwa na umuhimu mkubwa katika jamii ikashindwa kufanya vizuri, hivyo wamejipanga kuifanyia maboresho.
“Hapa Handeni kuna shule ilikuwa maarufu sana ya Kideleko ni ya miaka mingi na imekuwa Ikifanya vizuri sana mkoani hapa, lakini una changamoto ya uchakavu wa miundombinu yake, tunakwenda kuifanyia ukarabati iweze kuwa katika hali nzuri,”amesema Mwenyekiti huyo.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Albert Msando, amesema kuwa upo umuhimu wa shule hizo kuboreshwa Ili ziweze kuendana na mazingira ya sasa ya utoaji wa elimu, kwani zilikuwa ni msaada mkubwa kwa jamii.
Miradi mingine ya Jumuiya ya wazazi ambayo inahitaji kufanyiwa maboresho ni pamoja na viwanja vya michezo,majengo ya biashara ambavyo vina uwezo wa kuingizia mapato chama hicho.