CCM yaridhishwa utekelezaji miradi ya bil 600/-

DODOMA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, kimeridhishwa na utendaji kazi wa serikali baada ya kutembelea na kukagua miradi saba ya maendeleo yenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 600.4 inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Kauli hiyo ilitolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Donald Mejitii alipoongoza Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Mejitii amesema timu yake imetembelea na kukagua miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya Sh 600,424,100,099 na kujiridhisha kuwa imetekelezwa kwa kiwango bora.

Advertisement

SOMA: https://www.tamisemi.go.tz/

“Tunapopita katika ziara zetu, pia tunaangalia uhusiano baina ya serikali na chama. Hapa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uhusiano huo ni mzuri na ndiyo siri ya mafanikio.

CCM hakuna sehemu tumeona tunakwamishwa na serikali. Kila mradi tulioukagua umejengwa vizuri na unavutia,” alisema. Wakati huo huo, aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kupunguza migogoro ya ardhi kutokana na ushirikiano baina ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma hivyo kupunguza migogoro ya ardhi. “Miongoni mwa ushahidi ni kwamba malalamiko yanayokuja ofisi ya CCM Mkoa wa Dodoma yamepungua sana.

Ushahidi mwingine ni juhudi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kulipa fidia wananchi waliokuwa wakidai,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde aliahidi kuchangia Sh milioni 15 ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Shule ya Sekondari Zuzu na Sh milioni tano na kununua viti na meza kwa Shule ya Msingi Iyumbu.

SOMA: Wabunge wapitisha bajeti Wizara ya Ujenzi

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema timu yake ipo timamu katika kutekeleza miradi ya maendeleo na yote ipo sawa. Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dodoma ilitembelea mradi wa ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa na matundu 10 ya vyoo Shule ya Sekondari Zuzu, ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Dodoma na mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje.

Walitembelea pia ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa Msalato, ujenzi wa kituo cha afya Ilazo, mradi wa maji Nzuguni na ukarabati wa vyumba 10 vya madarasa Shule ya Msingi Iyumbu.

/* */