Chama, Dube, Abuya kunufaisha serikali mil 8/-

UHAMISHO wa wachezaji wa kimataifa wa Yanga, Cleatus Chama, Prince Dube na Duke Abuya utainufaisha serikali mamilioni ya fedha.

Ada za vibali kwa wachezaji wa kimataifa kutoka nje ni dola za kimarekani 500 sawa na sh milioni 1.3 lakini mchezaji wa kimataifa akitoka klabu moja kwenda nyingine kiwango kinapanda hadi dola 1000 sawa na sh milioni 2.67.

Msajili wa Vyama vya Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Evordy Kyando ameiambia Dailynews Digital  kuwa sababu ya kiwango cha uhamisho wa ndani kuwa kikubwa kuliko uhamisho wa nje kuja ndani ni gharama kutofautiana.

Advertisement

Soma: Usajili 2024: Chama amwaga wino Jangwani

Akitolea mfano kuwa uhamisho wa kumtoa mchezaji nje una gharama nyingi na watu wengi kwa maana ya mawakala lakini ule wa ndani ni rahisi hauna gharama nyingi ndio maana kiwango ni kikubwa.

Kwa maana hiyo uhamisho wa wachezaji watatu wa Yanga tu Chama aliyetoka Simba, Dube aliyotoka Azam na Abuya aliyetoka Singida utaipa serikali zaidi ya sh milioni nane. Bado uhamisho wa kimataifa nao utawaingiza fedha zaidi.

Sio kwa Yanga tu, bali klabu zote 16 zinatakiwa zifanye hivyo kwa kuwalipia wachezaji wao vibali vyote vya kufanya kazi.

“Mchezaji yeyote anayeingia nchini na kufanya kazi ana wajibu wa kisheria wa kulipiwa, Kuna malipo ya aina tatu na miongoni mwao ni kibali na kwa mujibu wa Sheria za BMT namba 49 toleo la mwaka 2002 na kanuni za uendeshaji kupitia tangazo la serikali namba 739 la mwaka 2020 zimebainisha mchezaji yeyote wa kigeni anapoingia nchini lazima alipiwe kiwango hicho cha fedha,”amesema.

Kyando amesema ada hizo haziwahusu wachezaji pekee bali hata viongozi wote wa benchi la ufundi au  watendaji waliotoka nje ya nchi kuja kufanya kazi kwenye klabu wanapaswa kulipiwa.

Amehimiza klabu zote kuhakikisha zinatekeleza Sheria kwa kuwalipia vibali kabla ya kuanza kwa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Championship na First League.