DAR ES SALAAM;Mtoto Elisha Kigobanya mwenye umri wa miaka saba aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, ameruhusiwa baada ya kukaa hospitalini takribani miezi 11 kutokana na changamoto ya ukuaji ( Cerebral Palsy (CP)).
Mloganzila kwa kushirikiana na wahisani imemsaidia vifaa tiba mbalimbali mtoto huyo hali inayomlazimu kuhitaji uangalizi wa karibu katika kutatua changamoto za ugonjwa huo.
Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo kwa wazazi wa Elisha, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Mloganziala Dk Julieth Magandi, ameeleza kufurahishwa na maendeleo ya kiafya ya mtoto huyo na kuahidi kuwa hospitali itaendelea kuwa bega kwa bega katika kutoa ushauri wa kitabibu pale itakapohitajika.
“Ni jambo la kushukuru kuona afya ya mtoto Elisha inaendelea kuimarika na sasa ameruhusiwa, nachukua nafasi hii kueleza kwamba pamoja na wahisani wengine kutoa msaada wa godoro hewa (air mattress), pamoja na kitanda uongozi wa hospitali tumempatia msaada wa vifaa vya Oxygen Concentrator na Nebulizer mashine ambavyo atatumia kwa muda mpaka pale atakapokua havihitaji tena, “amesema Dk Magandi.
Kwa upande wake Baba mzazi wa Elisha, Kenneth Kigobanya ameushukru uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa ukarimu, upendo, matibabu na huduma zote za kiutu walizozitoa kwa mtoto wao tangu alipopokelewa hospitalini Septemba 2022.
“Kipekee napenda kuushukuru uongozi na watumishi wa Mloganzila kwa namna walivyopambana na kuhakikisha wanaokoa maisha ya mwanangu ambaye awali hali yake kiafya ilikua mbaya,’’ ameeleza Kigobanya.
Comments are closed.