Chaumma kutangaza wagombea ubunge

DAR-ES-SALAAM : CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kinatarajia kutangaza majina ya wagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu Agosti 24, mwaka huu.
Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma, Benson Kigaila (pichani) alisema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari. Kigaila alisema baada ya uteuzi huo taarifa na orodha ya majina ya walioteuliwa itatumwa kwa Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya kuendelea na taratibu zingine za uchaguzi.
“Baada ya taarifa kutumwa INEC wateule hao wataenda kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na INEC kwa wasimamizi wa uchaguzi wakiwa na barua ya utambulisho ya Katibu Mkuu tume itakuwa na orodha yao lakini wao watakuwa na barua za utambulisho kutoka kwa Katibu Mkuu,’’ alisema.
Aliongeza: “Kwa sasa wagombea ubunge popote walipo kwa sababu bado hawajateuliwa hawawezi kwenda INEC kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na INEC kwa sababu lazima kwanza uteuliwe na chama ndio uchukue fomu ya INEC”.
Kigaila alisema chama hicho kimekamilisha uteuzi wa majina ya wagombea wa nafasi ya udiwani katika kata 3,182 za Tanzania Bara kati ya kata 3,962 zitakazoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Alisema mchakato wa kuwapata wagombea katika kata 780 zilizobaki unaendelea, hivyo wanachama wenye nia ya kugombea nafasi ya udiwani kupitia chama hicho kwenda kuchukua fomu katika kata hizo. Kigaila alisema majina ya wagombea udiwani kupitia chama hicho yameshatangazwa, hivyo wagombea waende kuchukua fomu kwa wasimamizi wa uchaguzi wakiwa na barua ya utambulisho kutoka kwa Katibu wa jimbo husika.
“Tumeona tusicheleweshe watu wote kwa ajili ya kata chache ambazo zinaendelea na mchakato, hizo kata ziendelee zikikamilisha majina yataletwa katika sekretarieti iliyokasimiwa mamlaka ya teuzi wakateuliwa na wakaenda kuchukua fomu,’’ alisema.
Aliongeza: “Niwaombe makatibu wa majimbo, wilaya na mikoa wasaidiane kuhakikisha wagombea wetu wa udiwani bila kucheleweshwa wanapata barua za utambulisho na wanaenda kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na INEC’’.
Wakati huohuo Chama cha ACT Wazalendo kimefanya Kikao cha Kamati Kuu Maalumu cha kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea ubunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. SOMA: CUF, CHAUMMA kuzindua kampeni leo
Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman katika ukumbi wa Hakainde Hichilema Dar es Salaam jana na kilihudhuriwa na viongozi wa chama hicho akiwemo Kiongozi wa wa chama hicho akiwemo Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu.



