KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewaonya wakurugenzi wa halmashauri kutotumia magari yaliyotolewa kwa ajili ya usimamizi wa huduma.
Akiwa kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku 10 kwa Mkoa wa Dodoma, Chongolo amesema CCM imeelekeza serikali kuhakikisha ifkikapo Agosti mwishoni mwaka huu kila wilaya inapelekewe magari mawili ya wagonjwa na moja la usimamizi wa sekta ya afya.
“Maagizo yetu kwa Serikali iyaandike kuwa hili gari ni ya usimamizi na si la mkurugenzi kwasababu kuna tabia ya wakurugenzi anaondoka na gari la usimamizi eti anaenda kwenye kikao Dodoma au Morogoro huku huduma zinasimama, gari la usimamizi libaki kuwa la usimamizi litoe huduma na si vinginevyo.”
“Mkurugenzi kama hana gari, apande basi ili wananchi waendelee kuwa na uhakika wa huduma. Tufike mahali tuone umuhimu wa kuwahudumia wananchi hatutaona shida ya kutumia usafiri wa aina yoyote.
“Kama gari lako bovu gari la afya sio mbadala kwa ajili yako na vivyo hivyo kwa magari ya elimu au mengine yaliyopewa shughuli maalumu.” Amesema