WAFANYABIASHARA nchini na wananchi, wametakiwa kutumia vyema maonesho ya CTW Tanzania 2022, yaliyoanza jana ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, kwani ni fursa nzuri kwa biashara.
Akizungumza katika onesho hilo, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk.
Exaud Kigahe, alisema lina faida kubwa kwa nchi.
“China Trade Week (CTW) Tanzania 2022 ni mpango muhimu wa kuunganisha biashara ya kimataifa kati ya China na Tanzania, ni tukio la kwanza la mchanganyiko Dar es Salaam kwa kukutanisha wazalishaji wa kampuni 50 kutoka China na wafanyabiashara wengi kutoka Tanzania kimtandao B2B (Business to Business).
“Tumekuwa na uhusiano wa kindugu na China, ambao umefanya uwekezaji na ukuaji wa viwanda vingi vya kitanzania,” alisema.
Dk. Kigahe kila alipopita katika mabanda hayo, aliwahimiza wamiliki wa kampuni hizo kuja kuwekeza Tanzania, ili kuongeza pato la nchi na kuwapatia vijana ajira.
Pia aliwataka wafanyabiashara wa sehemu mbalimbali za Tanzania kuhudhuria onesho hilo, ili kupanua wigo wa biashara zao katika maonesho hayo yatakayomalizika kesho.
“Hii ni fursa ambayo wafanyabiashara mmeletewa, kupitia onesho hili unaweza kujifunza namna utengenezaji unavyofanyika, unaweza kuagiza na kununua, lakini pia unaweza kutoa mawazo yako namna unavyotaka bidhaa iwe, na tumetoa agizo kwa kampuni hizi kutengeneza na kuleta bidhaa zenye ubora tunaouhitaji, ” alisema.