Dabi ya Kariakoo yagusa wabunge

DAR ES SALAAM; MCHEZO wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na Simba uliopangwa kufanyika wikiendi hii Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam unazidi kugusa wadau mbalimbali wa michezo.
Leo Juni 11, 2025, baada ya Naibu Waziri wa Habari, Utqmaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, kumaliza kujibu swali la msingi la Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Hassan Kungu aliyetaka kujua mkakati wa serikali kuandaa Taifa Stars madhubuti itakayoshiriki fainali za Afcon mwaka 2027, ndipo suala la dabi ya Kariakoo likajitokeza.
Alianza Mbunge wa Makete, Festo Sanga aliyetaka kauli ya serikali kinachoendelea kuhusu mchezo huo, lakini baada ya Naibu Waziri kujibu swali hilo la nyongeza, Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson alimpa nafasi ya kuzungumza Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya.
“Mheshimiwa Esther Bulaya, hebu sema unayosema kwenye kisemeo,” alisema Spika Tulia na ndipo Mbunge Bulaya alisema: “ Nilikuwa nasema kuhusiana na taratibu na sheria ni pamoja na kupata ripoti kwa nini mchezo wa tarehe nane haukuchezwa.”
Kauli hiyo ya Bulaya ikamfanya Spika atamke:” Sasa wewe ulikuwa unakataza ushabiki, sasa hapo unataka ushabiki, haya wa Simba naye anayetaka kumjibu. Mheshimiwa Esther Matiko mjibu.”
Baada ya kupewa fursa hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu Esther Matiko, akasema:” Nashukuru mheshimiwa Spika kama alivyojibu Naibu Waziri, lazima tuheshimu kanuni ambayo ina guide mchezo wa mpira wa miguu na kukuza vipaji, tusiweke ushabiki.”