DARAJA LA MAGUFULI: Kichocheo cha biashara na uchumi EAC

“BARABARA nzuri na madaraja hayafanyi kazi ya kuunganisha maeneo pekee, bali pia huunganishja watu na fursa, watoto na shule, wakulima na masoko, kwa ujumla huchochea maendeleo ya nchi.”
Anasema Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akinukuu moja ya taarifa za Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wakati akiwasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Ujenzi katika Mwaka wa Fedha 2025/2026.
Ulega anasema ujenzi wa miundombinu imara kama barabara na madaraja ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa lolote duniani ikiwamo Tanzania. Katika wasilisho lake, analiomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuiidhinishia Wizara ya Ujenzi Sh 2,280, 195,828,000.
Anasema, “Kati ya hizo, Shilingi 90,468,270,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya wizara na taasisi na Shilingi 2,189,727,550,000 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.”
Kwa mujibu wa Ulega, utekelezaji wa miradi ya maendeleo unajumuisha fedha za ndani; zaidi ya Sh bilioni 980.5 zikiwamo takribani Sh bilioni 688.756 kutoka Mfuko wa Barabara na zaidi ya Sh bilioni 520.466 kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali.
Katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 unaomalizika mwishoni mwa mwezi ujao, Wizara ya Ujenzi ilitengewa Sh 81,407,438,000 ikiwa ni bajeti ya matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, Sh 76,588,233,000 zilikuwa bajeti ya mishahara na Sh 4,819,205,000 zilikuwa kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Kwa mujibu wa Ulega, hadi Aprili 2025 Sh 63,506,309,562 zilikuwa zimepokewa. Anasema, “Bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo iliyotengwa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa Wizara ya Ujenzi ilikuwa Shilingi 1,687,888,714,000.” Kati ya fedha hizo, Sh1,141,803,989,000 ni fedha za ndani na Shilingi 546,084,725,000 ni fedha za nje.

“Kati ya fedha za ndani zilizopokewa, Shilingi 482,085,328,011 ni kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali na Shilingi 462,796,255,323 ni za Mfuko wa Barabara.”
Katika hotuba yake, waziri huyo anasema bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 inazingatia misingi na maono mbalimbali ya serikali na taifa kwa ujumla ikiwamo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022-2025/2026) na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020.
Mengine ni Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 pamoja na ahadi za viongozi wakuu wa serikali.
Kwa kuzingatia umuhimu wa miundombinu mbalimbali ya usafiri na usafirishaji, makala hii inajikita katika faida za Daraja la J.P. Magufuli (Kigongo-Busisi) katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza baina ya wilaya za Sengerema na Misungwi.
Daraja hilo ni mradi mkubwa wa miundombinu uliojengwa kuunganisha wilaya hizo sambamba na kuunganisha mkoa huo na Geita ili kuchochea manufaa ya kiuchumi na kijamii. Ikumbukwe kuwa, wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani mwaka 2021, ujenzi wa daraja ulikuwa umefikia takribani asilimia 25. Ulega analiambia Bunge,
“Kutokana na changamoto za kutetereka kwa uchumi wa duniani baada ya kuibuka janga la Uviko (Ugonjwa wa Virusi vya Korona-19) kulikuwa na wasiwasi kuwa ni wapi tutatapa Shilingi bilioni 539.28 kukamilisha mradi huo.” Mradi huo umegharimu Sh bilioni 610.
“Naomba kutumia fursa hii kutoa pongezi na shukrani kubwa kwa Rais Wetu, Samia Suluhu Hassan ambaye si tu amelipa fedha zote hizo kwa mkandarasi kwa wakati, bali pia amekamilisha mradi wa ujenzi uliokuwa ndoto ya mtangulizi wake.”
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali wakiwamo wakazi wa Mwanza, kukamilika kwa ujenzi wa daraja kutakuwa faraja kwa namna mbalimbali kwa Watanzania kiuchumi na hata kijamii. Vyanzo vinanukuliwa mtandaoni vikitaja baadhi ya faida za daraja hilo kuwa ni pamoja na kuboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo mbalimbali ikijumuisha ya kibiashara kwa kupunguza muda wa safari.
Vyanzo vinasema daraja hili limepunguza muda wa safari kati ya Kigongo na Busisi kwa kutoa njia ya moja kwa moja bila kutumia kivuko. Kuhusu suala la muda, Ulega anasema, “Baada ya daraja kukamilika, muda wa kuvuka daraja unatarajiwa kupungua kutoka saa mbili, hadi wastani wa dakika tatu.”
“Aidha, daraja hili linategemewa kuongeza shughuli za kiuchumi ndani na nje ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani.” Anaongeza: “Daraja hili pia litakuwa mojawapo ya alama na fahari ya taifa letu kwani kwa urefu wake wa kilometa 3.2, litakuwa daraja refu zaidi katika ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Kuanza kutumika kwa daraja hilo kutarahisisha usafirishaji wa mizigo kati ya Mwanza na Geita jambo litakakoboresha biashara na kuongeza ufanisi. Wakazi wa Kanda ya Ziwa wanasema muda utakaookolewa kutokana na matumizi ya daraja hilo utatumiwa na watu kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwamo za biashara, uzalishaji mali na utoaji huduma kwa jamii.
Hivi karibuni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) ilipofanya ukaguzi katika daraja hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonda alisema suala la gharama za kuvukia daraja hilo lipo katika mchakato ambao pamoja na mambo mengine, unaangalia kipi kilipiwe na kipi kisilipiwe.
Anasema daraja hilo litatumika kutoa huduma katika kipindi chote cha mwaka kwa saa 24 na kuwezesha mazao ya kilimo, samaki na bidhaa nyingine kufika sokoni kwa wakati. Mkazi wa Bukumbi Mwanza, Mwanaidi Magembe anazungumzia suala la malipo katika matumizi ya daraja hilo akisema, “Kama watu walikuwa wanalipia kivuko kwa kuchelewa, hakuna ubaya kulipia daraja kwa kuwahi namna hii.”
Uboreshaji miundombinu unatajwa kuwa moja ya mambo makubwa na muhimu yanayovutia wawekezaji na kuimarisha shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika kilimo, biashara na utalii.
“Baada ya kuanza rasmi kutumika kwa daraja hili, mambo hayo yataonekana na kufanyika sana,” anasema mmoja wa wataalamu wa uchumi mkoani Dar es Salaam.
Inaelezwa kuwa, utekelezaji wa mradi huo si tu kwamba utanufaisha Watanzania pekee kibiashara na kiuchumi hususani mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Mwanza, Geita, Kagera na Kigoma, bali pia nchi jirani za Rwanda, Uganda, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Burundi.
Kupanua Soko
Taarifa katika bajeti ya wizara hiyo hiyo inabainisha kuwa, vivuko vyote vilivyokuwa vinatumika katika eneo la Kigongo-Busisi vitapelekwa katika maeneo mengine nchini ambayo yana uhitaji. Daraja hili pia linatajwa kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na huduma nyingine muhimu kwa wakazi wa maeneo yanayolizunguka.
Chanzo kimoja kimeandika kuwa, daraja hilo litatoa njia salama ya kuvuka Ziwa Victoria ikilinganishwa na kivuko (feri) kinachoweza kuwa katika hatari inapotokea hali mbaya ya hewa au ajali.
Kimsingi wadau wanasema matumizi ya daraja hilo yatatatua kero ya miaka mingi iliyosababisha vifo kutokana na ajali za majini na wagonjwa kucheleweshwa hospitali, kuchelewa kwa biashara na safari za wananchi.