DC Kubecha: Tatueni changamoto za wakulima
LUSHOTO:MKUU wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Japhari Kubecha amewataka maofisa ugani kuhakikisha wanatatua changamoto za wakulima wa wilaya hiyo.
–
DC Kubecha amesema hayo katika hafla ya kugawa vitendea kazi pamoja na usafiri kwa maofisa hao vilivyotolewa na serikali.
–
“Hakikisheni mnawatatulia wakulima matatizo yao, nawaomba mkavitunze vyombo hivi vya usafiri,”amesema DC Kubecha.
–
Ameipongeza Wizara ya kilimo kwa juhudi inazofanya katika mageuzi sekta ya kilimo nchini.
Akizungumza Mei 18 mwaka huu Mkuu huyo wa Wilaya ya Lushoto amewaelekeza maofisa kilimo wa wilaya hiyo kuandaa mpango mkakati wa kilimo kwa miaka mitano ambao utaonesha kila kata kuwa na zao la kimkakati la biashara.
Alikuwa akizungumza katika kikao na wadau wa kilimo, umwagiliaji na maofisa ugani wa wilaya hiyo ambapo Kubecha amewataka pia maofisa kilimo kwenye maeneo kuwasikiliza na kutatua changamoto za wakulima.
“Ipo mikakati ya kitaifa, lakini tukasema na sisi tuandae mikakati ya wilaya, naamini sio kila mahali panakuba kila zao, naamini iko kata fulani zao fulani litakuwa linakubali, muhimu tuweke mikakati hapa namna gani kata hiyo tunaenda kuweka msukumo kwenye zao fulani,”alisema.
Pia Kubecha aliwataka maofisa umwagiliaji wa wilaya hiyo kufanya utafiti wa kina wa kubaini maeneo yanayotakiwa kuongezwa tija kwenye umwagiliaji.
“Mliacha maeneo ya mifereji, muende mkafanye tathmini tuandike andiko nilishatoa maelekezo kupeleka kwenye tume ya umwagiliaji tuone namna gani mifereji tunaisadia kuwekewa bajeti na kufanyiwa upembuzi na ukarabati,” alisema DC Kubecha.
Mei 2, 2024 Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha ya Wizara yake kwa Mwaka 2024/2025 ambapo katika hotuba yake amesema katika mwaka ujao wa fedha, wizara itaendelea kutekeleza vipaumbele vitano (5) vya mwaka 2023/2024 kwa kukamilisha miradi iliyoanza mwaka 2022/2023, 2023/2024 na kuanza miradi mipya.
Bashe alisema wizara inalenga kukuza Sekta ya Kilimo kwa upande wa mazao kufikia asilimia 5 kuchangia asilimia 20 katika Pato la Taifa, kuendelea kuchangia asilimia 100 ya upatikanaji wa chakula na kuongeza mauzo ya mazao nje ya nchi hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3 ambapo malengo hayo yatafikiwa kwa kutekeleza vipaumbele sita na mikakati 27.
Aidha, Amesema wizara imeongeza kipaumbele kimoja na hivyo kufanya vipaumbele vya mwaka 2024/2025 kuwa sita (6) vitakavyotekelezwa kupitia mikakati 27.
Pia, Bashe ameainisha vipumbele hivyo ni pamoja na kuongeza tija na uzalishaji (Increase Productivity and Production), kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake kwenye kilimo,kuimarisha usalama wa chakula na lishe, kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na mauzo ya mazao nje ya nchi, kuimarisha maendeleo ya ushirika pamoja na kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika uendelezaji wa Sekta ya Kilimo.