DC Mgomi aendelea kuhamasisha lishe bora

SONGWE: MKUU wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, ameendelea na kampeni ya kuhamasisha lishe bora kwa watoto kupitia Siku ya Afya na lishe ya Kijiji (Saliki) ambapo amefanya ziara katika Kata ya Sange.
Katika ziara hiyo, DC Mgomi alishiriki na kuzungumza na wananchi, akisisitiza umuhimu wa lishe bora kama msingi wa kuimarisha afya na ustawi wa watoto wilayani humo.
Akizungumza na wazazi na walezi katika kata hiyo, DC Mgomi aliwapongeza wakina mama wa Sange kwa kuonesha uelewa na juhudi katika kuhakikisha watoto wao wanapata lishe bora sambamba na malezi yenye kuzingatia maadili ya Kitanzania. Alieleza kuwa hatua hiyo ni kielelezo cha uzalendo na mchango wa moja kwa moja katika kuijenga jamii imara na yenye tija kwa taifa.
Aidha, alitoa wito kwa wazazi wote wa Wilaya ya Ileje kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama, yenye upendo, lishe bora, na maadili mema.
Alisisitiza kuwa msingi wa Taifa imara unaanzia katika familia bora, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika ili kuandaa kizazi bora cha baadaye.