MKUU wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amewataka wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa shule mpya inayojengwa Kata ya Mtoa kumaliza ujenzi huo kwa wakati ili Januari 2025 wanafunzi waanze kusoma hapo.
Mwenda ameyasema hayo Oktoba 24,2024 alipofanya ziara katika kata hiyo kwa lengo la Kukagua maendeleo, kusikiliza na Kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Kwa upande wake, Athumani Kaliki amemweleza Mkuu wa Wilaya walipokea mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari ila wanashangaa kuona kuna wenzao wawili wanadai eneo.
“Tunajiuliza kila mradi unapokuja Mtoa huwa kuna shida mpaka tunajiuliza sisi watu wa Mtoa tuna dhambi gani? Kila mradi tukipata tunakuwa na vikwazo na kusuasua na sisi mkuu wetu wa wilaya tunapenda maendeleo na ndiyo maana tumejitoa kutoa nguvu kazi kama kuleta mchanga,maji,”alieleza Athumani Kaliki.
SOMA: Mil 348/- kuwezesha mikopo halmashauri Iramba
DC Mwenda amewataka wananchi wilayani Iramba kujitolea maeneo yao kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayoletwa na serikali katika maeneo yao.
SOMA: Mwenge wa Uhuru wakagua miradi ya Sh Bil 5 Iramba
Akisoma taarifa fupi ya mradi wa ujenzi wa shule hiyo, Mkuu wa Shule ya Mtoa ambaye ni msimamizi wa mradi Mwalimu Basil Mkanga amemueleza DC Mwenda kuwa wamepokea zaidi ya Sh milioni 544 Kupitia SEQUIP na mradi utakuwa na uwezo wa kuwahudumia wanafunzi 320 kutoka Vijiji vya Mgela,Mtoa na Msai. Jamii imechangia mchanga tripu 104 zenye thamani ya Sh milioni 4.1