DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050 inataka nchi ifi kie maendeleo endelevu yanayozingatia uhifadhi wa mazingira.
Rasimu ya sera hiyo inaeleza dira hiyo inataka ipunguze uzalishaji wa hewa ukaa na kujenga uwezo wa kuhimili na kukabili mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa rasimu hiyo, dira hiyo imetaja maeneo yatakayozingatiwa katika kukabili mabadiliko ya tabianchi ni uhifadhi wa bioanuai, uhifadhi wa ardhioevu na rasilimali maji, udhibiti wa uchafuzi wa mazingira, usimamizi endelevu wa ardhi pamoja na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
Rasimu hiyo inaeleza mfumo wa uhifadhi wa bioanuai katika ikolojia mbalimbali unahusisha ulinzi endelevu wa viumbe hai na mimea ikiwa ni pamoja na uoto wa asili wa savana, misitu ya mvua, mikoko na viumbe wa baharini na wanyamapori.
Inaeleza uhifadhi huo hufanyika katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba, maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori wa wananchi ambayo yametengwa maalumu kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na uwindaji uliodhibitiwa.
Pia, hifadhi za misitu zinazolenga kuhifadhi mazingira ya misitu, hifadhi za bahari zilizolenga kuhifadhi maisha ya baharini kwa pamoja maeneo haya yaliyohifadhiwa yana ukubwa wa takribani asilimia 32 ya ardhi ya nchi, ambayo ni muhimu kwa uhifadhi wa bioanuwai.
Ilisema utenganishaji wa kaboni, udhibiti wa uchafuzi wa mazingira na uhifadhi wa rutuba ya udongo vitu muhimu kwa maisha ya binadamu na ustawi wa kitaifa.
Rasimu inaeleza bioanuai hiyo imeiwezesha Tanzania kushika nafasi ya 10 kimataifa kwa wingi wa viumbe vinavyohifadhiwa, inayotambuliwa na shirika la kimataifa linalosimamia viumbe walio hatarini kutoweka duniani.
Inaeleza kuwa licha ya hayo viumbe hai vinakabiliwa na vitisho kutokana na shughuli za binadamu ukiwemo ujangili, ukataji haramu wa miti, uvamizi wa kilimo, na upanuzi wa miji, biashara haramu ya wanyamapori, hasa ya pembe za ndovu na nyama ya pori, inazidisha shinikizo na kusababisha upotezaji wa bioanuwai.
Katika kukabili athari hizo, rasimu hiyo inaeleza Tanzania inatekeleza sera zinazolenga kuimarisha kwa uhifadhi wa mazingira na viumbe hai ikiwemo Sera ya Taifa ya Mazingira (2021), Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (2004), Sera ya Wanyamapori Tanzania (2007), Sera ya Taifa ya Misitu (1998) na Sera ya Ufugaji Nyuki (2007) pamoja na sheria zake.
Inasisitiza kuwa na mifumo ya mipango ya ushiriki wa jamii za wenyeji katika uhifadhi wa bioanuwai na shughuli za kiuchumi, ushirikiano wa kimataifa na uzingatiaji wa makubaliano ya kimataifa ya uhifadhi wa bioanuwai yatakayoonesha dhamira ya Tanzania katika kulinda urithi wake asilia na kuchangia katika juhudi za uhifadhi duniani.
Rasimu inaeleza juhudi endelevu ni muhimu kupunguza athari, kuimarisha hatua za uhifadhi na kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu wa bioanuwai kwa vizazi vijavyo.
Dira inatarajia ifikapo 2050 Tanzania itakuwa kinara duniani katika uhifadhi wa bioanuai katika mazingira ya asili pamoja na kuwa na mifumo madhubuti ya ulinzi wa wanyamapori na mimea dhidi ya ujangili, uvunaji haramu wa magogo, uvamizi wa viumbe na kuhakikisha uendelevu kwa vizazi vijavyo.
Inatarajia pia Tanzania itakuwa kinara katika matumizi endelevu ya bioanuai kwa manufaa ya uchumi wa nchi na maendeleo ya jamii na kutambua thamani halisi ya bioanuwai katika pato la taifa.