Dk Biteko kufungua Mkutano Usimamizi wa Intaneti

DAR ES SALAAM; NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk, Doto Biteko ndiye atakayefungua Mkutano wa 14 wa Jukwaa la Usimamizi wa Intaneti Afrika (AfIGF) Mei 29, mwaka huu Dar es Salaam, HabariLEO limebaini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Dk Nkundwe Mwasaga amebainisha hayo leo wakati akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya Shule ya Usimamizi wa Intaneti (School of Internet Governance) Afrika uliofanyika jana katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Katika ufunguzi huo wa sehemu ya kwanza ya mkutano huo, Dk Mwasaga amesema mafunzo hayo ni fursa kwa vijana Watanzania wanaoshiriki kwa kuwa nao watafundisha wenzao kuhusu usimamizi wa intaneti na fursa zilizopo katika matumizi sahihi na salama ya intaneti zikiwamo za kiuchumi.
“Tanzania tuna uchumi mkubwa wa kidijiti; tena unaokua; ni uchumi wa watu takribani milioni 62…” amesema Dk Mwasaga.
Akaongeza: “Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 34 ni takriban milioni 23; hili ni jeshi kubwa la kiuchumi kama watachangamkia fursa za intaneti ipasavyo kwani hata… Soko Huru la Afrika lina fursa nyingi na biashara kupitia zina fursa nyingi katika intaneti.”
Amesema mafunzo hayo ni fursa mihumu kwa Tanzania.
Naye Mkurugenzi wa Miundombinu ya Mawasiliano katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Leo Magomba amesema mkutano huo mkubwa wa Mei 29 hadi 31, mwaka huu utafunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko.
Aidha, amesema kipindi maalumu kitaongozwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kujadili mambo mbalimbali zikiwamo sera za mawasiliano na uchumi wa kidijiti.
“Tanzania tutajifunza kwa wenzetu kutoka nchi nyingine ndani na nje ya Afrika na wao watajifunza mengi kutoka Tanzania…” amesema Magomba.
Kwa mujibu wa Magomba, mkutano huo kwa ngazi ya Afrika unalenga kuendeleza mijadala ya pamoja kuhusu matumizi ya intaneti, anga salama, usalama wa mtandao, mawasiliano ya mtandao, usimamizi wa intaneti, uchumi wa kidigiti, akili mnemba na haki za kidijiti.
Awali katika utambulisho wa ujio wa mkutano huo ilielezwa kuwa, utakutanisha washiriki wapatao 1,200 kutoka Afrika na mataifa mbalimbali duniani kutoka serikalini, mashirika ya kiraia, sekta binafsi, wasomi na jumuiya za kiufundi kama jukwaa muhimu yanayounda mustakhbali wa kidijiti Afrika.